Tuliona ya kwamba watu wanaokuzunguka wanataka wewe ushindwe, hasa pale unapopanga kufanya mambo makubwa, ambayo wao hawakuweza kufanya.

Lakini hili halitokei kwa wengine pekee, hata kwako pia linatokea. Kuna nyakati ambapo unatamani mtu ashindwe au apate changamoto kwenye jambo analofanya. Hasa pale anapojaribu kufanya jambo kubwa, au anapopingana na kile ambacho unamshauri afanye.

Ni hali inakujia kutaka ashindwe au akutane na changamoto ili ajifunze au aone kwamba ulikuwa sahihi. Lakini hata akishindwa au akikutana na changamoto bado haikuongezei wewe chochote.

Kuondokana na hali hii watakie watu mema, watakie watu furaha kwenye maisha yoyote ambayo wao wamechagua kuishi. Heshimu kile ambacho wamechagua kufanya na watakie mafanikio na furaha. Na siyo kuwatakia kinafiki, ile unawaambia utafanikiwa wakati moyoni unataka washindwe, hapana. Hapa unahitaji kuwatakia mema kutoka ndani ya moyo wako, na siyo lazima uwaambie.

Kwa kufikiria mema ya wengine kuna faida kubwa kwako kwa sababu unakuwa na mtazamo chanya ambao unakuwezesha kuziona fursa nzuri zaidi kwenye maisha yako. lakini unapowatakia wengine mabaya, unakuwa hasi na kuzikosa fursa nzuri za kwenye maisha yako.

SOMA; UKURASA WA 522; Kila Mtu Anataka Wewe Ushindwe…

TAMKO LANGU;

Kuna wakati ambapo nimekuwa natamani watu washindwe au wakutane na changamoto ili wajue siyo rahisi au niwe sahihi kwamba walipaswa kutekeleza ushauri niliowapa. Lakini nimegundua hilo halinisaidii chochote zaidi ya kuniweka upande hasi. Kuanzia sasa nitakuwa nawatakia watu mema na furaha katika kile walichochagua kufanya, hii itaniwezesha kuwa chanya na kuzioana fursa nyingi zaidi.

NENO LA LEO.

Kuna wakati ambapo unatamani watu wakutane na changamoto au washindwe ili wajue kwamba mambo siyo rahisi au wajute kwa nini hawakufuata ushauri wako.

Lakini hilo halikusaidii wewe chochote, na badala yake inakufanya uwe hasi zaidi na hivyo kushindwa kuziona fursa nzuri zinazokuzunguka.

Watakie watu mema, watakie watu furaha na watakie watu mafanikio. Kufanikiwa kwao ndiyo kufanikiwa kwako, fikiria upande chanya na utapata mengi chanya kwenye maisha yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.