Kuna watu ambao wametuzunguka, kwenye kazi zetu, biashara zetu na hata maisha yetu ya kawaida ambao huwa wanakera. Yaani watu hawa unatamani hata wasingekuwa karibu na wewe kwa sababu kila kitu wanachofanya wanakukera sana. Wengine wanaweza hata kukuharibia siku yako na kukupotezea muda wako kutokana na mambo ambayo wanayafanya.

Watu hawa wanaokera kuna ambao wanafanya kwa makusudi ili kukuzuia wewe kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako. Pia kuna ambao hawajui hata kama wanakukera, wao wanafanya kile ambacho ni muhimu kwao.

Kitu kibaya tunachoweza kukipata kutoka kwa watu hawa ni pale tunapojiruhusu kuharibu siku zetu au kupoteza muda wetu kwa sababu ya watu hawa. Nasema sisi ndiyo tunajiruhusu kupoteza muda, kwa sababu kile wanachokifanya wengine hakina nguvu ya kubadili chochote kwako, ila tafsiri yako kwa kile kilichofanyika ndiyo inakufanya uharibu siku yako na kupoteza muda wako.

Tunahitaji njia bora ya kuweza kukabiliana na watu hawa ili wasiendelee kuwa kero kwetu. Na njia bora sana kwetu ni sisi kuwaelewa watu hawa na kutoruhusu hisia zetu ziharibu amani yetu. Elewa kwamba kuna watu hawa ambao kile wanachokifanya hakiendani na wewe, iwe wanajua au hawajui. Chagua kutokuangalia hiki zaidi na angalia ni vitu hani vingine wanavyofanya watu h6awa ambavyo vinaendana na wewe na vina manufaa kwako.

Pia kumbuka hata wewe mwenyewe unawakera watu, kwa mambo ambayo unachagua kuyafanya kuna watu ambao hayaendani nao na hivyo kukereka. Elewa kwamba siyo kila mtu atakubaliana na wewe na pia wewe huwezi kukubaliana na kila mtu.

Dhibiti hisia zako na usiwe mtu wa kukasirika kila mara kutokana na mambo ya wengine ambayo yanakukera. Unapokuwa unakasirika unajiharibia mwenyewe mambo yako kwa kujipotezea muda, yule unayemkasirikia huenda hata hajui au hajali. Kuwa mwamuzi wa mwisho wa hisia zako, usikubali ziyumbishe na kila kitu ambacho wengine wanafanya au wanashindwa kufanya.

Watu wanaokera hawapaswi kuwa chanzo cha wewe kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri kwako. Kuwa makini na dhibiti hisia zako, maisha ni yako na maamuzi yote ni yako.

TUPO PAMOJA,

Kocha.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Usiruhusu Vitu Vidogo Viharibu Siku Yako.