Katika maisha yetu kuna maamuzi ambayo huwa tunafanya na tunakuwa tumekosea, kwa kukosea maamuzi hayo tunapata matokeo mabaya, yaani mambo yanakwenda vibaya. Sasa hapa ndipo penye hatari kubwa sana.
Hapa kuna hatari kubwa kwa sababu mambo yanapoanza kuharibika, huwa tunakaza na kuchukua hatua haraka sana, na kwa bahati mbaya sana hatua tunazochukua huwa zinaharibu zaidi hali ya mambo. Tunajikuta tunaharibu mambo ziadi ya yalivyokuwa awali na hapa ndipo unapoanza mteremko wa kila kitu kuharibika.
Najua umewahi kuona hili kwa wengine na hata kwako wewe binafsi. Mtu anafanya maamuzi ya kibiashara ambayo yanakuwa siyo mazuri, anapokazana kuyarekebisha ndiyo anaharibu zaidi. Au mtu anafanya maamuzi ya kikazi ambayo yanaleta matatizo na anapojaribu kuchukua hatua ndiyo anaharibu zaidi.
Njia ya kuondokana na hali hii ni kufikiri kwa kina kabla ya kukimbilia kufanya maamuzi. Kuona kama maamuzi hayo yatakuwa bora au la. Hii ni rahisi kufanya, na siyo inayowapelekea wengi kwenye kuharibu zaidi.
Kinachowapelekea wengi kuharibu zaidi na hivyo kutengeneza makosa makubwa ni kutokukubali kwamba wamefanya makosa. Au kama wamekubali basi kutaka kuyaficha ili wengine wasijue. Pale ambapo mtu anashindwa kukubali kwamba amefanya makosa hasa anapopata matokeo mabovu, anachukua hatua ya kufanya kile kile ambacho kimemletea matokeo mabovu. Kwa sababu hakubali njia aliyotumia ndiyo mbovu, anarudia kuitumia tena kwa ubora zidi na hivyo kupata matokeo mabaya zaidi.
Wengine wanajua wamekosea lakini wanataka kuficha ili isionekane na wengine. Na hapa wanajikuta wanaharibu mambo kuliko hata wasingeficha. Nafikiri umewahi kuona mtu ambaye alifanya kosa dogo na kuogopa kusema hivyo kudanganya. Na baada ya hapo akawa anaendelea kudanganya makubwa na makubwa zaidi ili kuficha lile kosa lake dogo la mwanzo. Mwishoni anajikuta ana makosa mengi ameyafanya ambayo yameharibu sana kuliko ambavyo ingekuwa kama angekuwa muwazi kwenye kosa la kwanza.
Kubali kwamba umekosea na pia kuwa tayari kuwaambia wale wanaohusika kwamba umefanya makosa na kisha fanya maamuzi sahihi kwenye hali yoyote ambayo unapitia.
Mambo yanapokwenda vibaya, zuia majaribu yanayokujia ya kufanya mambo ambayo yatafanya hali iwe mbaya zaidi. Badala yake fikiri kwa kina na ukiona mchango wako kwenye mambo kwenda vibaya na kuwa mkweli na mwaminifu. Utajifunza mengi na pia utaondokana na hasara kubwa unayoweza kutengeneza kwenye kazi yako, biashara yako au maisha yako kwa ujumla.
Kufunika moshi usionekane, hakuzimi moto, bali kunaufanya moto ulete uharibifu mkubwa zaidi kwa sababu wengine hawataona kama kuna moto na kuja kutoa msaada.
TUPO PAMOJA.
KOCHA.
SOMA; Mambo yanapokwenda vibaya kwenye biashara yako fanya hivi.