Mambo yanapoharibika, au yanapokwenda kinyume na matarajio yetu, huwa tunakimbilia kuangalia ni nini kimesababisha. Na kwa haraka sana huwa tunatafuta ni kitu gani cha nje ambacho kimechangia mambo kwenda tofauti na matarajio yetu.

Biashara inapopata hasara, au inaposhindwa kuleta faida uliyotarajia kupata, mawazo yako yote yanakwenda kwenye kitu cha nje ambacho kimechangia biashara kutokwenda sawa. Hapa utaona ushindani mkali wa kibiashara, wateja ambao siyo waaminifu, wafanyakazi ambao ni wasumbufu na kadhalika.

Unapopata matatizo kwenye ajira yako, iwe ni kwa ajira kuisha au kushindwa kupata kile ambacho ulitegemea kupata kwenye ajira, ni rahisi sana kuona sababu za nje kwa nini hupati unachotaka. Na hapa utaona bosi ambaye hajali, wafanyakazi wenzako ambao wanakuonea wivu, hali ya uchumi ambayo siyo nzuri na mengine kama hayo.

Sababu za nje ni moja ya mambo yanayopelekea vitu kutokwenda kama vilivyopangwa, lakini siyo sababu pekee. Kuna sababu za ndani pia, ambazo ni sababu muhimu sana na zimekuwa changamoto kwa wengi. Zinakuwa changamoto kwa sababu wengi hawataki kuzikubali na hivyo zinaendelea kuwatesa.

Kwa changamoto yoyote unayopitia kwenye maisha yako, kazi yako au biashara yako, wewe mwenyewe una mchango kwenye changamoto hiyo. Wewe mwenyewe kuna jinsi ambavyo umechangia changamoto hiyo mpaka imeendelea kuwepo. Kuna sababu za ndani yako ambazo zinapelekea changamoto hiyo kuwepo na hivyo kukuzuia wewe kupata yale matokeo ambayo ulikuwa unayatarajia.

Hivyo basi pale unapojikuta kwenye changamoto, pale unapopata matokeo ambayo ni tofauti na matarajio yako, usiishie tu kuangalia nje, bali angalia na ndani yako. Anza kwa kuangalia ndani yako na jiulize ni kwa namna gani wewe mwenyewe umechangia ile changamoto ambayo upo. Angalia ni vitu gani ambavyo umefanya au umeshindwa kufanya na vimechangia changamoto hiyo kuwepo.

Ukiweza kufikiri hivi kwenye kila changamoto unayopitia, utaweza kutatua zaidi ya nusu ya changamoto zote ulizonazo bila hata ya kuhangaika na watu wengine. Mara nyingi huwa tunataka wengine wabadilike ila sisi wenyewe hatupo tayari kubadilika, na wakati kubadilika kwetu wenyewe ndiyo suluhisho la kila kitu kwenye maisha yetu.

Tujitathmini na tuone mchango wetu kwenye changamoto zinazopitia, na tuchukue hatua ili kuwa na maisha bora zaidi kila siku. Kumbuka maisha bora yanaanza na wewe mwenyewe popote ulipo kwa sasa. Cheza nafasi yako.

TUPO PAMOJA,

KOCHA.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DIFFICULT CONVERATIONS (Mbinu Za Kujadili Mambo Magumu Na Muhimu Kwako)