Moja ya hisia kali sana kwetu binadamu ni hofu.

Hofu inaweza kutuzuia kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yetu na pia hofu inaweza kutufanya tuchukue hatua ambazo siyo bora kwetu.

Kwa watu kujua hili, wamekuwa wakitumia hofu kunyanyasana wao kwa wao. Pale ambapo mtu anataka ufanye kitu na hana njia ya kukushawishi ufanye, hatua ya mwisho kwake ni kutumia hofu ili ufanye. Wakati mwingine pale mtu anapotaka ufanye kitu ambacho hakina umuhimu wowote kwako bali kwake yeye anatumia hofu kuhakikisha unafanya.

Hofu hizi zimekuwa zinatumika kila eneo la maisha yetu, kuanzia kwenye jamii, kwenye biashara, kwenye kazi na kila mahali.

Kwenye jamii hofu imekuwa inatumika kuwalazimisha watu kufanya vitu fulani. Watu wanahofia kutengwa au kukosa ushirikiano na wengine na hivyo kulazimika kufanya vitu ambavyo havina manufaa yoyote kwao. Wakati mwingine wanaweza kunyimwa huduma muhimu mpaka pale watakapokubaliana na kile ambacho wengine wanataka mtu akubaliane nacho.

Katika biashara hofu imekuwa inatumika kukusukuma ununue hata kama kitu siyo muhimu kwako. Watu watakuambia hii iliyobaki ni ya mwisho, huwezi kupata tena. Au watakuambia bei imeshushwa leo tu kesho bei itakuwa juu. Au watakuambia watu wengi wanaitaka nafasi hii, ukichelewa hutaipata. Hofu kama hizi zinakusukuma kuchukua hatua ambazo siyo bora sana kwako.

Kwenye kazi hofu ndiyo zimetawala kila kona. Kuna mambo mengi mtu analazimika kufanya kwenye kazi ili tu aendelee kuwa kwenye kazi hiyo. Na kwenye ulimwengu huu wa sasa ambapo ajira zimekuwa chache kuliko wahitaji, mtu atajikuta akifanya vitu ambavyo havina mchango wowote kwake wala kwa kazi yake ili tu atetee nafasi yake ya kazi. Wenye mamlaka ya kuajiri wamepata nafasi nzuri ya kuwanyanyasa wengine kwa sababu wanajua ajira ni ngumu na hivyo wanawapa majukumu mengi huku mshahara ukiwa kidogo kwa kuwapa hofu kwamba kama hawataki waache, wahitaji wa ajira ni wengi.

Ufanye nini?

Kama upo upande wa kunyanyasika, usikubali kuendelea kunyanyasika, badala yake fikiri kwa kina kabla hujafanya maamuzi. Usikubali hofu iendelee kutumika kukusukuma kufanya maamuzi. Kuwa na misingi yako unayoisimamia kwenye maisha na hakikisha kile unachokubali kinaendana na misingi hiyo. Kama upo kwenye ajira ambayo unyanyasaji ni mkubwa na huwezi kuchukua hatua haraka, basi fanya maandalizi ya kuondoka kwenye ajira hiyo kwa sababu mambo hayatakuwa mazuri, haijalishi unatamani kiasi gani yawe mazuri. Anayekunyanyasa ataendelea kukunyanyasa, mpaka pale wewe mwenyewe utakapoamua kuchukua hatua.

Kama upo kwenye upande wa unyanyasaji, acha mara moja. Unaweza kutumia hofu kupata matokeo unayotaka, lakini hii itakuwa mara moja au mara mbili, baadaye itaharibu mahusiano mazuri na wale unaowapa hofu. Badala yake tumia hamasa kuwafanya watu wachukue hatua. Wafanye watu wachukue hatua kwa sababu wanaona ni muhimu kwao na siyo kwa sababu wanahofia wasipochukua watadhurika.

Usikubali kunyanyasika kwa hofu na pia usinyanyase wengine kwa kutumia hofu.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; UKURASA WA 312; Giza Sio Kitu…. Hofu Sio Kitu…..