Kila kitu kwenye maisha yetu kina gharama. Kuna gharama fulani unatakiwa kulipa ili uweze kupata kile ambacho unataka. Gharama hii inaweza kuwa kwenye mfumo wa fedha, muda, juhudi na hata utu binafsi. tunalipa gharama kwenye kila eneo la maisha yetu, kuanzia kwenye familia, kazi, biashara na hata kwenye jamii tunazoishi.

Kwenye biashara, bei tunayopanga kuuzia bidhaa au huduma zetu nayo inakuja na gharama zake. Wengi huwa hawajui gharama hizi na kujikuta kwenye wakati mgumu. Kuna wafanyabiashara wanaoamini kuweka bei ndogo kunavutia wateja wengi na hivyo kupata faida kubwa. Wapo pia wanaoamini kuweka bei kubwa kunawavutia wateja walio makini na kuweza kutengeneza faida nzuri. Lakini hizi zote zinakuja na gharama zake.

Gharama ya bei ndogo.

Kuweka bei ndogo kunakuja na gharama zake, tena zinaweza kuwa gharama kubwa sana. Gharama hizi ni kama ifuatavyo;

Urahisi wa wengine kuweza kuiga kile ambacho unafanya na hivyo ushindani kuwa mkubwa. Pale ambapo unashusha bei ili kuwavutia wateja wengi zaidi, pia unavutia wafanyabiashara wengine ambao watakuja na bei ndogo zaidi.

Gharama nyingine ni kuwa na wateja wengi ambao unashindwa kuwapa huduma nzuri kila mmoja na hivyo kutowaridhisha na kuwa rahisi kwao kwenda sehemu nyingine kupata huduma hizo.

Pia kuwa na bei ndogo kunaweka picha kwenye akili za watu kwamba kile unachouza thamani yake ni ndogo na hivyo kutokukiamini sana kutokana na bei yake ndogo.

Gharama ya bei kubwa.

Kuweka bei kubwa pia siyo kinga ya gharama, bado utaingia gharama kama mfanyabiashara pale unapoweka gharama kubwa. Zifuatazo ni baadhi ya gharama hizo;

Kuhitajika kutoa thamani kubwa sana. Pale ambapo mteja anatozwa bei kubwa, matarajio yake yanakuwa makubwa sana. Hivyo ni jukumu lako kama mfanyabiashara kuhakikisha matarajio hayo ya mteja yanafikiwa.

Gharama nyingine ni kuwapoteza baadhi ya wateja ambao wanaogopa kuja kwenye biashara yako kwa sababu ya sifa ya bei kubwa. Wengine wangeweza kabisa kupata kile wanachotaka kwa bei nzuri, lakini kwa kuwa biashara yako inasifika kwa bei kubwa, wanaogopa hata kuja.

Pia inachukua muda mpaka mtu afanye maamuzi ya kununua kama gharama ni kubwa. Mtu anahitaji kuaminishwa kweli anachofanya ni bora kwake ili asipoteze fedha zake.

Ipi gharama bora?

Hakuna gharama bora zaidi ya mwenzake, bali kuna gharama bora kwa kila mtu, kulingana na malengo na mipango yake. Kikubwa toa huduma bora sana kwa wateja wako ili wafurahie, waridhike na muendelee kufanya kazi kwa pamoja.

Kila la kheri.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; BIASHARA LEO; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Kwenye Upangaji Wa Bei.