Kwenye kila eneo la maisha, kuna watu ambao wapo chini. Watu ambao wana maisha magumu sana kuliko wengine wote. Watu ambao kipato chao ni kidogo sana na wakati mwingine ni watu ambao wanafanya mambo mengi sana. Lakini bado wapo chini na wanaendelea kuwa chini. Ni kitu gani kinawafanya waendelee kuwa chini?
Wao wenyewe.
Watu waliopo chini, wako pale kwa sababu hawajataka kweli kuondoka pale walipo. Wanaweza kuwa hawapapendi, ila hawajapata hasira za kutosha kuwaondoa pale. Hawajapachukia hasa kiasi cha kutangaza vita na kuwa chini. Wanaona siyo mbaya sana na hivyo kuendelea kuwa pale.
Wakati mwingine wanakuwa wameshaona pale walipo ndipo mahala pao. Wanaona pale ndipo nyumbani kwao na hivyo zinapokuja juhudi zozote za kuwaondoa pale hawafurahii.
Utawajuaje watu ambao wamechagua kuendelea kuwa chini?
Sikiliza kauli zao, angalia matendo zao.
Kauli zao zinakwenda kama hivi;
Sisi ni masikini…
Sisi ni wanyonge…
Sisi tunaonewa…
Sisi hatujaliwi…
Utasikia kauli nyingi za kuwafanya waonekane wao wanakandamizwa, kama vile kuna mtu ambaye ana jukumu la kuwatoa pale walipo. Mbaya zaidi watu hawa wanadanganyika pia na mifumo iliyopo, ya kijamii na kiserikali.
Kwenye matendo yao utaona kitu cha tofauti kabisa;
Muda wa kazi yeye atafanya vitu vingine ambavyo haviendani na kazi…
Anachelewa kuingia kwenye kazi na anawahi kuondoka…
Akipata mshahara anatumia wote na kuanza kukopa, mshahara unaokuja analipa madeni na kuendelea kukopa…
Biashara anayofanya akipata faida anatumia yote, akikosa anatumia hata sehemu ya mtaji…
Akipewa kazi anatafuta njia ya kuiba au kunufaika zaidi ya wengine…
Anapenda kuongea kuliko kufanya…
Hizo ndizo tabia za watu ambao wamechagua kukaa chini, watu ambao wamegoma kabisa kuyasaka mafanikio. Na huenda wanakuwa wamedanganywa kwamba kuna mtu atawaletea mafanikio wanayotaka, labda ndugu, wazazi au serikali.
Ninachojua ni kwamba wewe rafiki yangu siyo mmoja kati ya watu hawa, na kama kwa bahati mbaya ulikuwa umeanza kuwa na tabia zinazopelekea kuendelea kuwa chini, ziache mara moja.
Miliki maisha yako, jua kile unachotaka, jua jinsi ya kukifikia na weka juhudi kukifikia, usikubali kelele za wengine zikuzuie, maisha yako ni jukumu lako, hakuna atakayeweza kukuletea kile unachokitaka, unakipigania wewe mwenyewe.
Kila la kheri rafiki, tukatae kuwa chini, na tukutane kileleni, kwenye kilele cha mafanikio.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; UKURASA WA 14; Kataa Kupokea Chochote Kizuri, Na Kubali Hiki…