Hakuna kitakachotokea kwenye biashara yako mpaka pale utakapofanya vitu hivi viwili muhimu sana na kwa mfuatano sahihi.
Kwanza muuzie mtu kile unachotoa, iwe ni huduma au bidhaa.
Pili mtu aridhishwe na kile ulichomuuzia.
Hii ndiyo misingi inayobeba biashara yako. Mengine yote unayofanya kwenye biashara kama hayaipeleki biashara kwenye misingi hii miwili muhimu, unapoteza tu muda.
Hakuna biashara kama hakuna mtu anayenunua, siyo kusema atanuna, bali kununua, kutoa fedha yake aliyoipata kwa jasho na kukupa wewe ili umpe bidhaa au huduma unayotoa, huku akijua anaweza kuipata sehemu nyingine na siyo kwako tu.
Hakuna biashara endelevu na inayopata mafanikio kama watu hawaridhishwi na kile wanachonunua, lazima wanachonunua kitatue changamoto zao, ili warudi tena na wawaambie wengine kuhusu uwepo wa biashara yako.
Kila wakati jiulize kwenye biashara yako, je unachofanya kinapelekea mtu anunue? Na je mtu akinunua atakuwa tayari kuja kununua tena? Ukijiuliza maswali haya utatoa bidhaa na huduma bora sana na pia utapata mbinu nyingi za kumfikia mteja wako ili aweze kununua.
Haya ndiyo mambo mawili ambayo yanapaswa kukuumiza kichwa wewe mfanyabiashara, na siyo vitu kama wazo lipi ni bora au mtaji napata wapi. Kama una kitu ambacho watu wanakihitaji, na ukaweza kuwapatia, hutakuwa na muda wa kufikiria wazo la biashara liweje au mtaji unapata wapi.
Peleka nguvu zako kwenye maeneo haya mawili ya biashara yako, mauzo na ubora. Mengine yatakwenda sawa kama haya yapo sawa.
Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.