Ukiwasikiliza watu jinsi wanavyokueleza maisha ni magumu kwao, unaweza kupata huruma sana kwa namna ambavyo maisha siyo “fair” kwao. Utaona huruma sana kwa nini kila baya linawafika wao tu. Watakueleza jinsi walivyo wema, jinsi ambavyo wanakazana kufanya, lakini hali au watu wengine wanakuja kuharibu kila kitu.
Watakuambia jinsi ambavyo waajiri wao wanawanyanyasa, wanawalipa kidogo na kuwatumikisha kama punda, huku hawajali kabisa ile kazi wanayoifanya.
Watakuambia jinsi ambavyo biashara zao zinakutana na changamoto, watu wanawakopa hawarejeshi, wengine wanawatengenezea maneno ya majungu ili kuharibu biashara zao.
Watakueleza jinsi ambavyo watu kwenye familia zao wanawanyanyasa, watakuambia namna ambavyo watu wamewazushia mambo mbalimbali ambayo wao hawajawahi kufanya kabisa.
Ukiwasikiliza, unaweza kuumia sana, na kuona hii siyo sawa, mtu huyu mwema hivi kwa nini mabaya yote haya yatokee kwake tu.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Changamoto Za Kuondoka Kwenye Vifungo Vya Maisha Na Kupata Uhuru Wa Maisha.
Leo nataka nikuambie kitu kimoja, umekuwa unadanganywa na watu hao unaowasikiliza, hakuna mtu mwema sana ambaye kila baya linamfika yeye tu. Kwa nafasi kubwa mabaya yanawatokea watu kwa sababu wameyakaribisha, iwe kwa kujua (consciously) au kwa kutokujua (subconsciously). Huamki tu asubuhi maisha yako yakaanza kuwa mabaya, bali kuna mambo ambayo unafanya au hufanyi na yanapelekea maisha yako kuwa magumu.
Anayekuambia ajira yake inamtesa na bosi wake anafanya maisha yake kuwa magumu, hatakuambia jinsi ambavyo anafanya kazi zake kwa mazoea, hatakuambia jinsi ambavyo kinachomsukuma kufanya kazi ni kwa vile tu analipwa. Pia hatakuambia ya kwamba hatekelezi majukumu yake mpaka atishiwe. Na mwisho kabisa, hatakuambia kwamba hajiendelezi kwenye kazi hiyo zaidi ya kuwepo kuwepo tu.
Anayekuambia kwamba biashara yake inamsumbua, hatakuambia jinsi ambavyo anaifanya biashara hiyo kwa mazoea, hatakuambia kwamba hana msingi wowote anaousimamia kibiashara. Hata kuambia jinsi ambavyo anawakopesha watu hovyo, hata wale ambao hawawezi kabisa kulipa kile wanachokopa. Pia hatakuambia maamuzi ya kizembe anayofanya kwakuendeshwa na hisia.
Hakuna mtu mwema ambaye mabaya yote yanamtokea yeye tu, bali kila mtu anatengeneza mazingira ya mambo mabaya kumtokea. Jukumu letu kwenye maisha siyo kutafuta nani mchawi, bali kuangalia ni jinsi gani tumefanya makosa mpaka tukajikuta pale ambapo tupo kwa sasa, kisha tufanye marekebisho.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)