Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Ni imani yangu kwamba uko vizuri na maisha yako yanaendelea kuwa bora kila siku kupitia falsafa mpya ya maisha unayojijengea. Hatujifunzi tu falsafa hii mpya ya maisha ili tuwe tunajua sana, bali tunajifunza ili kuitumia kuboresha maisha yetu. Hivyo chochote unachojifunza, hakikisha unaweza kukitumia kwenye maisha yako, na kuyafanya kuwa bora zaidi. Na siyo lazima uchukue kila kitu kama unavyojifunza, badala yake kiboreshe ili kiendane na maisha yako na mazingira yako.
Karibu kwenye makala ya leo ya falsafa mpya ya maisha ambapo tunakwenda kuangalia kitu kimoja ambacho kinamwathiri kila mmoja wetu hasa kwenye dunia ya sasa ambayo inakwenda kasi sana. Kama kuna kitu kimoja ambacho maisha hayakosi basi ni changamoto, uwe huna fedha kuna changamoto zako, uwe na fedha una changamoto zako. Uwe umeajiriwa una changamoto zako, uwe huna ajira una changamoto zako. Iwe una biashara una changamoto zako. Kila maisha yana changamoto zake, na hakuna ambazo ni nafuu ya nyingine, ila sisi wenyewe ndiyo tunaweza kuamua changamoto ziwe nafuu kwetu au ziwe kali.
Changamoto hizi tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku, zinapelekea sisi kupata msongo wa mawazo, au kwa kiingereza inaitwa stress. Stress siyo mbaya, ni moja ya vichocheo vya sisi kuweka juhudi zaidi. Pale ambapo unatakiwa kumaliza kazi fulani kabla ya siku kuisha, unakuwa na stress ambayo itakufanya uache kufuatilia vitu vingine na ukazane na kazi hiyo tu mpaka iishi. Pale ambapo mtoto wako amepata ajali, unaweza kumbeba na kukimbia naye mpaka hospitali apate huduma, bila ya kujali uko kwenye hali gani, hapa stress inakusaidia kupata nguvu za ziada kufanya vitu. Na kwa wale ambao ni wanafunzi, kabla ya mitihani kukaribia unaweza kusoma mada moja kwa siku nzima, huna haraka, lakini mtihani unapokuwa karibu, stress inakufanya usome mada moja ndani ya saa moja, na huenda ukaelewa haraka kuliko kipindi ambacho huna mitihani. Hivyo kwa njia moja stress ina msaada kwenye maisha yetu.
Ila siyo stress zote zina msaada kwenye masiha yetu, na hata zile stress zinazotusaidia, zikizidi zinakuwa tatizo, stress zinapozidi zinasababisha ugonjwa wa akili unaujulikana kama sonona (Depression) na hata magonjwa mengine ya kawaida yanaweza kuchochewa na stress, kwa sababu wakati wa stress, kinga ya mwili inapungua sana hivyo kuuweka kwenye hatari ya kushambuliwa na magonjwa.
Leo kupitia falsafa yetu mpya ya maisha tunakwenda kujifunza jinsi ya kuondokana na stress zisizo na maana kwetu na jinsi ya kudhibiti zile stress ambazo zina msaada kwetu ili zisitupeleke kwenye magonjwa.
Ili kuweza kudhibiti stress kwanza kabisa unahitaji kugawanya mambo yote yanayotokea kwenye maisha yako katika makundi mawili makuu.
Kundi la kwanza ni mambo ambao yapo nje ya uwezo wako. Haya ni yale mambo ambayo huwezi kufanya chochote kuyabadili, yapo kama yalivyo na huwezi kufanya chochote kuyazuia au kuyabadili.
Kundi la pili ni yale mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako, haya ni mambo ambayo unaweza kufanya kitu kuyabadili au kuyazuia. Ni mambo ambayo yanaweza kubadilika au kuimarika kwa wewe kuchukua hatua fulani.
Haya ni makundi makubwa mawili ambapo ukiweza kuyaelewa vizuri, utapunguza asilimia 80 ya stress unazokutana nazo sasa. Kwa sababu watu wengi huwa wanajipa stress kwa mambo ambayo hawawezi kuyabadili kwa namna yoyote ile.
Hiyo ni hatua ya kwanza, kugawa mambo kwenye makundi mawili. Hatua ya pili ni kuyaacha yale ambayo yapo nje ya uwezo wako, kutokujiumbua nayo kabisa na kuchukua yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako ili kuyafanyia kazi.
Yale mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako nayo unayagawa kwenye makundi mawili;
Kundi la kwanza ni yale mambo unayoweza kuyaathiri moja kwa moja. Yaani hapa unaweza kufanya kitu na kubadili hali unayopitia. Mambo haya yapo chini yako moja kwa moja na unaweza kuyabadili au kuyazuia kabisa.
Kundi la pili ni yale mambo ambayo huwezi kuyaathiri moja kwa moja. Haya huwezi kuyabadili au kuyazuia kwa kuchukua hatua fulani, badala yake unaweza kuchukua hatua ambayo inaweza kupelekea kubadili mambo hayo, lakini siyo moja kwa moja, kwa sababu kuna mambo na watu wengine wanaohusika.
Kwenye ile asilimia 20 iliyobaki kwenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wako, unayoweza kuathiri moja kwa moja ni asilimia 5 na usiyoweza kuathiri moja kwa moja ni asilimia 15. Hivyo mpaka hapa tumeshaondoa asilimia 95 ya mambo ambayo yamekuwa yanakupa stress na kubaki na asilimia 5 ambayo unaweza kuyafanyia kazi na ukabadili maisha yako.
Tuangalie mifano ya jinsi stress zinazotusumbua kila siku tunavyoweza kuziweka kwenye kundi sahihi na kuchukua hatua.
- Upo kwenye foleni na umechelewa unakoenda.
Moja ya mambo yanayowapa watu wengi stress ni kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu huku waichelewa kule wanakoenda. Iwe ni kazini au kwenye kikao, hali hii inaleta stress kubwa. Hatua unazoweza kuchukua badala ya kuumia na stress ni kuanza kuchambua.
Kwanza acha kutamani foleni hiyo iende haraka, hilo ni jambo ambalo lipo nje ya uwezo wako, achana nalo kabisa, halitasaidia chochote.
Fikiria kama kuna hatua unayoweza kuchukua ili kuondoka kwenye foleni hiyo, labda kama unaweza kushuka kwenye gari na kupanda pikipiki ambayo itakuwahisha haraka kwa sababu haikai sana kwenye foleni. Kama unaweza fanya hivyo. Kama huwezi kuchukua hatua hiyo basi achana kabisa na kuumia kwa kuwa kwenye foleni hiyo, kaa tulia na subiri mpaka utakapofika unapokwenda, kama umewakwamisha wengine waombe samahani, lakini ondoka na somo moja kubwa sana, wakati mwingine wahi kuondoka ni bora uwahi saa nzima kabla ya muda unaotakiwa kufika kuliko kuchelewa dakika kumi.
Hapa umeichambua hali inayokupa stress, umekubaliana na usichoweza kubadili na umepata hatua ya kuchukua. Ukiwa umewahi na kuna foleni, unakuwa na muda mzuri wa kufanya mambo yako mengine, labda kusoma au kusikiliza kitabu ukiwa kwenye foleni.
- Una mambo mengi ya kufanya lakini muda haukutoshi.
Jambo jingine linalowapa watu stress ni muda, na hii ndiyo changamoto kubwa ya dunia ya sasa. Kuna mambo mengi ya kufanya kuliko muda tulionao wa kufanya mambo haya. Hivyo tunajikuta muda umeisha na hatujafanya tunachotakiwa kufanya.
Kuondokana na stress ya aina hii tunachukua hatua ile ile, kuweka mambo kwenye sehemu yanapohusika. Je ni vitu hani vipo ndani ya uwezo wetu na vipi ambavyo havipo ndani ya uwezo wetu. Vile ambavyo vipo ndani ya uwezo wetu, ni vipi tunaweza kuathiri na vipi hatuwezi kuathiri.
- Mtu amekuahidi atafanya kitu halafu hajafanya.
Hiki ni chanzo kikubwa cha stress kwa watu wengi. Mtu anakuahidi atafanya kitu, na wewe unategemea sana kitu hicho mwisho wa siku hafanyi kama alivyoahidi. Labda ni mtu unamdai na akakuahidi atakulipa siku fulani, na wewe ukawa umewaahidi wengine utawalipa siku hiyo, lakini siku inafika na hatekelezi alichoahidi, hii inakuharibia na wewe kwenye yale uliyowaahidi wengine. Unaweza kupata stress kubwa sana, lakini lazima uanze kuipangilia, je kwa kuwa na stress inasaidia chochote? Jibu ni hapana, bado unabaki hujalipwa. Sasa hapa unaanza kufikiria ni njia zipi za kumbana mtu huyo akulipe, au kama hutaki usumbufu uachane naye mpaka pale atakapokulipa. Na hapa ondoka na somo kubwa kwamba usiamini kwa silimia 100 kile unachoahidiwa, lolote linaweza kutokea hivyo ni bora kuwa na mpango mbadala.
Katika kugawa mambo kwenye makundi yale matatu, haya hapa ni mambo yanayoingia kwenye kila kundi;
Mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu;
Jambo lolote kuhusu kesho, lipo nje ya uwezo wetu, hakuna ajuaye kesho.
Jambo lolote kuhusu hali ya hewa, jua, mvua, baridi, joto, upepo hivi vipo nje ya uwezo wetu.
Mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu ila hatuwezi kuyaathiri moja kwa moja;
Jambo lolote ambalo mtu mwingine anatakiwa kufanya maamuzi kama mwajiri au mteja.
Tabia za watu wengine.
Matokeo ya kitu chochote tunachofanya, hasa kwenye mashindano na watu wengine.
Mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu na tunaweza kuyaathiri moja kwa moja;
Mawazo yetu.
Matendo yetu.
Tabia zetu.
Hisia zetu.
Ukiweza kudhibiti haya manne ambayo yapo chini ya uwezo wako na unaweza kuyaathiri, basi unaweza kudhibiti msongo wa mawazo kwenye maisha yako.
Usikubali stress ziendelee kutawala maisha yako, dhibiti stress zote unazopitia ili uweze kuwa na maisha bora.
Kila la kheri katika kujijengea falsafa mpya ya maisha,
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita kupata utaratibu.
Kupata vitabu vya kujisomea ili kuongeza maarifa na kuhamasika tembelea www.mobileuniversity.ac.tz