Rafiki yangu Tumainiel Kimaro anaandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba; waambie watu ukweli na watatumia kila rasilimali waliyonayo kukupinga. Watakuja na ushahidi kwamba unachowaambia siyo kweli. Ila waambie watu uongo na watakuja wakishangilia, watakubaliana na wewe na wala hawatahoji.
Hii ni kweli kabisa, ukitaka kuwapoteza watu, ukitaka kuwafukuza watu waambie ukweli. Lakini ukitaka kuwavuta watu, waambie uongo.
Unajua ni kwa nini? Kwa sababu ukweli ni mchungu, ukweli ni mkali, ukweli haubembelezi. Na watu hawapendi uchungu, hawapendi ukali wanapenda kubembelezwa. Ni tabia ya asili kabisa ya binadamu.
Kuna makundi matatu ya watu ambayo yameweza kutumia hali hii vizuri sana, wameweza kuitumia kujikusanyia watu wengi, ambao wanakubaliana nao na kuwatumia kufikia malengo yao.
Makundi hayo ni;
- Wanasiasa.
- Matapeli.
- Viongozi wa dini.
Waambie watu ya kwamba matatizo yao yamesababishwa na uvivu wao, uzembe wao na ujinga wao na watakupinga kwa nguvu zao zote. Watakuja na kila aina ya ushahidi kwamba matatizo yao siyo wao wameyasababisha. Lakini waambie matatizo yao hawajayasababisha wao bali ni serikali, au wapinzani, au ndugu au wazazi, au shetani, watakubaliana na wewe na watafurahi sana, hawatahoji mara mbili.
Waambie watu ya kwamba ili kufanikiwa wanahitaji kuweka juhudi kubwa sana kwenye kazi zao, wanahitaji kujitoa sana, wanahitaji kutokwa machozi jasho na damu ndiyo wafanikiwe, watakukatalia, watakuambia wewe hujui. Ila waambie kuna njia rahisi ya kufanikiwa, kuna njia ya kutumia akili kijanja na ukafanikiwa bila ya kutokwa jasho, watakuja makundi kwa makundi wakitaka njia hiyo.
Ni jambo la kushangaza lakini ndivyo watu walivyo, hawataki kusikia ukweli, bali wanataka kusikia kile wanachotaka kusikia.
Na wale wenye ajenda zao wamekuwa wakitumia hilo, hawawaambii ukweli, bali wanawaambia kile wanachotaka kusikia, na wanawavuna wa kutosha.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kinachotuzuia Kuujua Ukweli Na Hivyo Kushindwa Kuwa Na Maisha Bora.
Wewe kama mwana mafanikio epuka hili kwa nguvu zako zote, hoji kila kitu, chunguza ukweli wa kila kitu, usishabikie tu kwa sababu kila mtu anashabikia. Upende ukweli na utafute ukweli, na kama inavyosemwa, ujue ukweli nao utakuweka huru.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)