Katika kitu chochote unachochagua kufanya kwenye maisha yako, upo uwezekano wa kushindwa. Hata kama utajiandaa kiasi gani, bado uwezekano wa kushindwa upo. Jambo hili ndiyo limekuwa linawazuia wengi kushindwa kuchukua hatua, kwa sababu ya uwezekano wa kushindwa au kufanya vibaya.

Wengi hutaka kusubiri mpaka pale wanapokuwa na uhakika kwamba hakuna uwezekano wa kushindwa. Lakini hakuna wakati mtu anafikia hatua hiyo na hivyo kuwafanya wengi wasichukue hatua kabisa.

Mara zote kuna uwezekano wa kushindwa, ila pia kuna uwezekano mkubwa kwa kushinda kama utajaribu kufanya kitu kuliko kutokufanya. Yaani iko hivi, japokuwa chochote utakachotaka kufanya upo uwezekano wa kushindwa, usipofanya ndiyo umeshindwa kabisa. Lakini ukiamua kufanya, kuna uwezekano mkubwa wa kushinda, wa kupata kile unachotaka.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).

Hivyo kwa vyovyote vile fanya kitu, kama utashindwa utakuwa umejifunza na kama utashinda utakuwa umepata unachotaka. Kuacha kufanya kwa hofu ya kushindwa, kunakufanya ushindwe moja kwa moja, kwa sababu usipojaribu hata kufanya, huwezi kupata chochote.

Upo uwezekano wa kushindwa na pia upo uwezekano wa kushinda kwa wale wanaofanya. Ila usipofanya una matokeo ya aina moja pekee, tayari umeshashindwa. Kuwa mtu wa kufanya kwenye maisha yako, utapata mengi kuliko asiyefanya.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)