Wingi na ubora ni vitu viwili vinavyokwenda pamoja, lakini kimoja ni muhimu zaidi ya kingine, kwenye maeneo mengi ya maisha yetu.

Kwenye wingi  tunaangalia kile kiasi halisi cha kitu wakati kwenye ubora tunaangalia sifa halisi au aina ya kitu hicho.

Je ni kipi kinahitaji kuanza, wingi au ubora? Tuangalie kwenye maeneo tofauti tofauti.

Kwenye kula, hata kama utakula ugali kilo nzima peke yako pamoja na mboga ya mchicha mara tatu kila siku, huwezi kuwa na afya bora. Ndiyo utashiba sana kwa sababu umepata wingi wa kutosha, lakini hakuna ubora. Unakuwa umekuwa chakula cha aina moja pekee, wakati unahitaji vyakula vya aina tofauti tofauti ili uwe na afya bora. Vile vile kupata vyakula vya aina tofauti tofauti lakini ukawa hushibi, bado huwezi kuwa na afya. Hivyo kuwa na afya bora, unahitaji wingi sahihi na ubora sahihi wa chakula.

Kwenye urafiki, unaweza kuwa na marafiki wengi sana, lakini hamna ukaribu wa kutosha, hapa una wingi lakini huna ubora, kwa namna hii hutaridhika na urafiki huo. Lakini unaweza kuwa na marafiki wachache ambao mna ukaribu wa kutosha na ukanufaika sana kwenye mahusiano yenu. Hapa ubora ni muhimu kuliko wingi.

Kwenye biashara, wateja wako wanahitaji kuwa wengi ili uweze kupata wateja bora. Unahitaji kuwaambia wengi sana kuhusu biashara yako, ndipo wachache waweze kuchukua hatua na kuwa wateja wako. Huwezi kusema unatafuta wateja bora kwa kuwaambia wachache pekee, bali unahitaji kuanza na wingi na ukachuja kupata wachache ambao ni bora na wanaendana na biashara yako. hivyo hapa wingi ni muhimu.

SOMA; Maadui Kumi(10) Wa Ubora Wa Hali Ya Juu.

Hivyo umeona maeneo ambapo wingi ni muhimu kuliko ubora, ubora ni muhimu kuliko wingi na eneo ambapo ubora na wingi vinakwenda pamoja. Hivyo unapofanya maamuzi kwenye maisha yako, fikiria kwenye wingi na ubora, na angalia kipi muhimu kuanza nacho.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)