Kuna njia mbili za kuyaendea haya maisha;

Unaweza kucheza salama, ukaenda ukinyata, usitake kuonekana, wala kukosea na ukawa na maisha ya kawaida sana, ambayo hata wewe huyafurahii. Na yale matatizo ambayo ulifikiri utayaepuka kwa kucheza salama, bado yakaendelea kukuandama.

Njia ya pili ni kucheza kwa viwango vyako, huogopi kukosea wala kuogopa kuonekana, unafanya kile ambacho unajua ni sahihi na muhimu kwako. Hata kama wapo wanaokupiga wewe unaendelea kufanya kwa sababu unajua ni muhimu kwako. Na kwa njia hii unaweza kufanya makubwa na maisha yako yakawa bora zaidi kila siku.

Jamii zetu zinatufundisha kucheza salama, twende kimya kimya, tufanye kile ambacho tumezoea kufanya, kile ambacho kila mtu anafanya, ili tusionekane tofauti. Tukionekana tofauti tutachekwa, tukijaribu makubwa tukakosea tutachekwa na kudharauliwa, hivyo tunalazimika kucheza salama, na tunakuwa katikati ya kundi kubwa la watu ambao wanayachukia maisha yao.

SOMA; NENO LA LEO; Umuhimu Wa Kuchepuka…

Kuna wachache ambao wanakataa kucheza salama, wanabisha kabisa kuingia kwenye mkumbo huu, wao wanaamua kuishi yale maisha yenye maana kwao, wanajaribu mambo makubwa na ya tofauti, wanashindwa na wakati mwingine wanafanikiwa. Tukiwaangalia tunawaonea wivu, tunawaona wao wana uthubutu, wana vipaji, wana bahati au wamependelewa.

Lakini ukweli utabaki kuwa ukweli, kwamba kila mtu atapata kile anachotafuta, na kuvuna kile anachopanda. Wanaocheza salama wataishia kuwa wa kawaida, wanaothubutu kwenda mbali zaidi watapata zaidi.

Je wewe umechagua nini?

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)