Kuna wakati ambapo tunakuwa tumepanga mambo yetu vizuri, halafu anatokea mtu na kuvuruga kila ambacho tumekuwa tunapanga.

Tunapata hasira kali juu ya watu wa aina hii au hali kama hizi, na hii ndiyo inatufanya tupoteze kile ambacho tulikuwa tunatafuta.

Hasira zinakufanya upoteze, haijalishi ni hali gani unapitia au umekutana na nani, usipoweza kudhibiti hasira zako, lazima utapoteza.

Wahenga walisema HASIRA HASARA, hii ni kwa sababu kila unapokuwa na hasira unashindwa kujidhibiti na kudhibiti hali unayopitia. Kupoteza udhibiti kunakufanya ushindwe kufanya maamuzi sahihi.

Tatizo kubwa zaidi kwenye kupoteza kupitia hasira ni pale ambapo wengine wanatumia hasira zako kujinufaisha. Kuna watu ambao tayari wameshakusoma na wanajua ni vitu gani unavyokasirika haraka, wanavifanya kwa makusudi ili ukasirike. Ukikasirika unafanya makosa au maamuzi mabovu ambayo yanawanufaisha wao zaidi.

Kama ambavyo wavuvi wanatega samaki, kwa kuweka wavu wa kuvulia upande mmoja, na kuwavuruga samaki ili wakimbilie kwenye mtego wao, ndivyo watu wanavyotumia hasira zako kukutega wewe.

Hivyo kitu pekee unachopaswa kukumbuka na kufanya kila unapojikuta kwenye hali ambayo hukuitegemea, ni kudhibiti hisia zako, usikimbilie kukasirika na kuchukua hatua ambazo zitakuumiza zaidi.

Unawezaje kuacha kukasirika haraka?

Hili ni swali na changamoto, kwa sababu kuna watu ambao wameshajichukulia wao ni wa kukasirika haraka. Na wakati mwingine kuna mambo yanatokea na kukuudhi mno, kiasi kwamba huwezi kujizuia bali kukasirika, tena sana. Lakini kumbuka kwamba wewe ndiye mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, wewe ndiye unayeweza kuruhusu chochote kitokee au kisitokee kwenye maisha yako.

Hivyo wakati wowote unapojikuta kwenye hali ya kukwazika au kuvurugwa, jipe angalau dakika tano za kutokufanya au kusema chochote. Tumia muda huo kufikiri kwa kina kile ambacho kimetokea, angalia kinakuumizaje na pia kinakufaidishaje. Kumbuka kila kinachotokea kina faida na hasara, hivyo fikiria pande zote mbili za hilo. Pia pumua taratibu na kwa kina, hii itakupunguzia kuwa na jazba.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kwa Nini Hisia Bado Zinatushinda Kudhibiti Na Namna Ya Kuzidhibiti.

Mara nyingi ukifikiri jambo lolote kwa kina, na kutokukimbilia kuhukumu au kutoa suluhisho, utaona namna bora ya kuchukua hatua. Nafikiri wewe mwenyewe ulishafanya maamuzi ambayo dakika tano baadaye uliyajutia, vipi kama ungejipa dakika tano kabla hujafanya maamuzi? Hakika ungefanya maamuzi bora zaidi.

Hata kama ni kwenye mabishano na mtu, kama unaona hakuna kufikia maelewano, jipe muda kabla hujatoa maamuzi yako. unapojipa muda na kufikiri jambo kwa kina, unajipa nafasi nzuri ya kufanya maamuzi bora.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)