Kuna watu wengi ambao huwa wanafikia hatua ya kuona maisha yao hayana thamani tena. Ni katika hatua kama hizi wanachukua maamuzi ambayo yanaharibu kabisa maisha yao. Wanakuwa hawajali tena, hivyo wanafanya mambo ya hovyo kama ulevi na wengine kufikia hatua ya kujiua kabisa.

Furaha ni haki ya maisha yako.

Inachukua nguvu kubwa sana kufikia hatua hii ya maisha, na ni nguvu ambayo ni sawa na ile ungeitumia kuwa na maisha ambayo yana thamani. Lakini kwa kuwa wengi huwa hawaelewi hili, na kwa kuwa jamii zetu pia hazielewi, tumejikuta tukijikuta tunashindwa kuona thamani kubwa ya maisha yetu.

Leo nataka nikukumbushe ya kwamba kila maisha yana thamani ya kuishi, bila ya kujali umetokea kwenye mazingira gani, na bila ya kujali unapitia nini kwa sasa.

Iko hivi, kila maisha yana pande mbili, kuna upande mzuri na kuna upande mbaya, hii ni kwa kila maisha, kuanzia tajiri mpaka masikini, kuanzia mfanyakazi wa ndani mpaka raisi wa nchi. Kuna mambo mazuri kwenye kila maisha na kuna mambo mabaya.

Wale wanaothamini maisha yao ni kuwa na furaha ni wale ambao wanaangalia yale mambo mazuri, hivyo wanakuwa na matumaini ya mambo kuwa mazuri zaidi kadiri siku zinavyokwenda.

Wale wanaodharau maisha yao na kukata tamaa ni wale ambao wanaangalia yale mabaya ya maisha yao na kuona hakuna namna maisha yao yanaweza kuwa mazuri. Hii inawafanya wazidi kuona mabaya zaidi.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Jinsi Ya Kuishi Maisha Yenye Maana.

Kwa sababu ni sheria ya asili kwamba kila mtu atapata kile anachotafuta, anayeangalia mazuri ataona mazuri zaidi, na anayeangalia mabaya ataona mabaya zaidi.

Kila maisha yana thamani ya kuishi, kila mtu anayo sababu ya kushukuru kwenye maisha yake. Angalia upande huu wa maisha yako na utakuwa na maisha bora kila siku.

Angalia ni kitu gani unashukuru kuwa nacho kwenye maisha yako, na shukuru, kila siku, utaona jinsi utakavyokuwa na mengi ya kushukuru.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)