Linapokuja swala la kuongeza mauzo ili kuongeza faida kwenye biashara, wafanyabiashara wengi huwa wanaangalia sehemu moja pekee, kuongeza wateja wengi zaidi.
Kuongeza wateja ni mbinu muhimu ya kibiashara kwa sababu biashara yako inaweza kuwafikia watu wengi zaidi. Na kadiri unavyokuwa na wateja wengi, ndivyo unavyotengeneza uhuru wa biashara yako.
Lakini kupata wateja wapya siyo kazi rahisi, kwanza unahitaji kuwafikia, wajue kama biashara yako ipo. Kisha unahitaji kuwashawishi wanunue kwako, unahitaji kuwashawishi wakuamini na wakati hawakujui kabisa. Hili ni zoezi ambalo linachukua muda, na linahitaji uvumilivu.
Kuna njia nyingine ambayo siyo ngumu sana itakayokuwezesha kuongeza wateja kwenye biashara yako. Njia hii inawatumia wateja ambao unao sasa kwenye biashara yako.
Uzuri wa wateja ulionao sasa kwenye biashara yako ni kwamba tayari wanakuamini, wanakujua vizuri hivyo huhitaji kutumia nguvu kubwa kuwashawishi.
Swali linalokuja ni je unapataje mauzo zaidi kwa wateja ulionao sasa? Mbona kama umeshawauzia kile wanachokitaka?
Hapa ndipo zinakuja mbinu mbili muhimu unazoweza kuzitumia kuongeza mauzo kwa wateja ambao tayari unao kwenye biashara yako.
Mbinu ya kwanza; CROSS-SELLING.
Hapa unawauzia wateja wako bidhaa ambayo inaendana na ile ambayo tayari wamezoea kununua kwako. Unatafuta bidhaa au huduma ambazo zinaweza kuuzwa kwa pamoja na unamwuzia mteja wako.
Kwa mfano kama unauza nguo, unaweza kuongeza na viatu, mabegi ya nguo na vitu vingine vinavyoendana na nguo.
Kila biashara ina vitu ambavyo vinaweza kuuzwa kwa pamoja na biashara hiyo, iangalie biashara yako kwa kina na utazioana fursa nyingi za kumuuzia mteja wako zaidi. Fikiria ni kipi ambacho mteja wako atahitaji kutumia na kile unachomuuzia sasa, kisha mpatie.
Mbinu ya pili; UP-SELLING.
Hapa unamuuzia mteja bidhaa bora zaidi kwa gharama ya juu zaidi ya alivyokuwa anapata kwako awali. Hapa unachofanya ni kuwa na matoleo au madaraja tofauti ya bidhaa au huduma unayotoa. Kisha kumpa mteja nafasi ya kupanda na kupata daraja la juu kabisa na hivyo kulipa zaidi.
Kwa mfano kama unauza vitu ambavyo vina bei tofauti, unaweza kuanza kumuuzia mteja mpya kile cha bei rahisi, kikishamsaidia na akataka zaidi, unaweza kumshawishi kununua cha bei ya juu ambacho ni bora kuliko cha kwanza.
Ukiangalia biashara yako vizuri, utaona njia nyingi za kuweza kuongeza thamani zaidi na kuwashawishi wateja wako kulipa zaidi ya kile wanacholipa sasa.
Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.