Nimekuwa nakuandikia na kukushauri kuhusu biashara kwa muda sasa, nafikiri unashangaa ninapokuambia ufukuze wateja. Kabla hujashangaa, soma kwa makini ili mwisho uweze kufanya maamuzi sahihi ya biashara yako.

Tatizo la wafanyabiashara wengi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa na tatizo moja, ambalo limekuwa linawasumbua sana na kuwazuia kukuza biashara zao. Tatizo hilo ni kutaka kila mtu awe mteja wa biashara zao. Wanafikiri kila anayepita na kuulizia basi ni lazima awe mteja wao. Na hivyo hutumia nguvu nyingi kujaribu kumshawishi kila mtu, mwishowe wanapoteza wateja wazuri.

Iko hivi, hata kama unauza soda, ambazo kila mtu anauza, siyo kila mtu ni mteja wako. Kuna aina fulani ya wateja ambao ni lazima uwawinde na kuwavutia kwenye biashara yako. Kuna sifa fulani ambazo unahitaji wateja wako wawe nazo ili biashara yako iweze kwenda vizuri. Na mara nyingi sifa hizo zinaanza na wewe binafsi.

Kama wewe ni mwaminifu, na unayejali sana kuhusu wateja wako, unahitaji kuwa na wateja ambao nao ni waaminifu, na ambao wanajali kuhusu wewe. Ukipata wateja ambao siyo waaminifu, au hawajali kuhusu biashara yako, watakusumbua sana na kukufanya uone biashara ni ngumu kupita kiasi.

Hivyo kitu muhimu sana kuzingatia ni kujenga wateja ambao wanaamini kile unachoamini wewe, wana sifa zile ulizonazo wewe, na utaendesha biashara yako kwa furaha na kuweza kuikuza.

Hivyo kama una wateja ambao hawaendani na zile sifa za biashara unayofanya, hawajali kile unachojali wewe, waombe tu waende sehemu nyingine. Wala usiwaambie vibaya, waambie tu kwa sasa huwezi kwenda nao na hivyo unawashauri wapate huduma zao sehemu nyingine. Kwa njia hii utabaki na wateja ambao wanathamini kile unafanya, na utakuwa na muda wa kuwahudumia vizuri.

Najua hii ni ngumu sana mara ya kwanza, hasa pale unapokuwa unafanya biashara inayohitaji wateja wengi, lakini niamini kwenye hili, kuna wateja ambao wanakurudisha nyuma mno. Kuna siku niliwahi kukuandikia kuhusu sheria ya 80/20, sheria hii inasema kwamba asilimia 80 ya faida unayopata kwenye biashara yako, inatokana na asilimia 20 ya wateja wako. Na asilimia 80 ya matatizo unayopata kwenye biashara yako, inatokana na asilimia 20 ya wateja wako. Sasa unaonaje ukawajua wale asilimia 20 ya wateja wako wanaokuletea faida kubwa na ukawapa huduma bora sana. Wakati huo huo ukawajua wale asilimia 20 ya wateja wako wanaokuletea matatizo na ukawafukuza?

SOMA; Fukuza Wateja Hawa, Ni Mzigo Kwako.

Kama kuna wateja ambao wanakukosesha usingizi, kwa namna walivyo wasumbufu, wanasema hiki ukifanya, wanakuja na kingine, kila unachofanya hawaonekani kuridhika, usiendelee kuwa nao, watakufanya ushindwe kutoa huduma bora kwa wateja wengine ambao wanakuamini wewe na wapo tayari kunufaika kupitia biashara yako.

Usitake kila mtu awe mteja wako, taka kuwa na wateja ambao mtakwenda vizuri kwenye biashara yako.

Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.