Kila kitu kwenye maisha yetu kinaendeshwa na mahusiano. Kuna mahusiano yetu na wengine, mahusiano yetu na sisi wenyewe, pia mahusiano yetu na mafanikio. Pale ambapo mahusiano ni mazuri, ushirikiano unakuwa mkubwa na mafanikio ni dhahiri. Lakini mahusiano yanapokuwa mabovu, ushirikiano unakosekana na inakuwa vigumu kufanikiwa.
Leo tuangalie mahusiano yetu na fedha, je ni mahusiano ambayo yanachochea ushirikiano ili kufanikiwa?
Kama ulikuwa hujui, kila mtu ana mahusiano fulani na fedha. Kuna watu ambao kwa mahusiano waliyonayo na fedha, wanavutia fedha zaidi kwenye maisha yao, wapo ambao wanafukuza hata zile fedha walizokuwa nazo.
Fedha huwa inaenda kule inakohitajika, inakoheshimika na kutumika vizuri kuzalisha fedha nyingi zaidi. Fedha hukimbia kule ambako haihitajiki, haiheshimiki na haizalishwi badala yake inatumiwa tu.
SOMA; Kitu muhimu kwa mteja wako kuliko fedha anayokupa.
Sasa hebu jiulize ni yapi mahusiano yako na fedha? Kutaka kila mtu anataka fedha, lakini je wewe unaitafuta fedha kwa njia sahihi? Njia ambazo zitakuletea fedha hizo kwa uhakika? Kwa sababu wapo wanaotafuta njia za mkato, hawa mara nyingi huishia kupoteza muda wako.
Kutaka tu fedha haitoshi kujenga mahusiano mazuri na fedha. Je ukishazipata unazitumiaje? Hapa ndipo ilipo siri kubwa ya mahusiano na fedha na mafanikio pia. Wapo ambao wakizishika fedha zinakoma zenyewe, kwa sababu ni matumizi juu ya matumizi. Hakuna cha ziada kinachofanyika zaidi ya kutumia. Na wapo wale ambao kwenye kila kipato wanachopata, wanatafuta njia ya kuzalisha zaidi, kwa kuwekeza kwenye maeneo ambayo yanaweza kuwapatia faida, hata kama ni kidogo.
Tengeneza mahusiano na fedha ambayo yanavutia fedha kwenye maisha yako, unathamini nguvu ya fedha na kuweza kuzitumia kutengeneza mafanikio makubwa. itumie fedha kama kifaa cha kukuwezesha kutengeneza maisha bora kwako na kwa wale wanaokuzunguka. Kwa njia hii utakuwa na ushirikiano mzuri na fedha zako.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)