Kwenye haya maisha, kuna utumwa ambao tunakuwa tumeingizwa bila ya sisi wenyewe kujua, tunakuja kustuka tayari tupo kwenye utumwa. Lakini pia upo utumwa ambao tunaununua sisi wenyewe, sisi wenyewe tunachagua kuwa watumwa wa watu wengine.
Katika aina hizi mbili za utumwa, huu wa kujinunulia mwenyewe ndiyo mbaya zaidi, kwa sababu wengi wanakuwa hawajui kama wapo kwenye utumwa. Wanaona ni sehemu ya maisha yao ya kawaida, kumbe wapo kwenye shimo kubwa la utumwa, linalowazuia kupiga hatua kwenye maisha yao.
Watu wanajinunulia utumwa, pale wanapoanza kujali sana kuhusu watu wengine wanachofikiri juu yao. Pale unapoanza kujali kwamba watu wanakufikiriaje, kiasi cha kushindwa kufanya baadhi ya mambo, hapo umejiingiza kwenye utumwa, wewe mwenyewe.
Ni kweli kwamba tunahitaji kujijengea heshima fulani mbele ya wengine, na kuna namna ambavyo tunategemewa kufanya mambo yetu, lakini hayo yanatakiwa yatoke ndani ya tabia zako mwenyewe, yaani unatakiwa kufanya siyo kwa sababu watu wanaona au watakuhukumu, badala yake unafanya kwa sababu ndivyo ulivyochagua kufanya.
Pale unapoanza kujiuliza hivi nikifanya hivi wengine watanichukuliaje, a watanifikiriaje, na kuhofia kwamba watakuona wa tofauti au wa ajabu, basi umenunua utumwa. Utashindwa kufanya jambo lolote muhimu kwako kwa sababu mara zote unawafikiria wengine, unajiuliza watakuchukuliaje, na unaogopa kujaribu mapya na makubwa.
Utumwa huu umeua vipaji vya watu wengi, na ndoto zao kubwa. Wapoa watu ambao walikuja na mawazo makubwa ya kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao, lakini baada ya kuwafikiria wengine, nguvu zote zimewaisha na kubaki wa kawaida. Wanaona ni bora wafanye kwa kawaida kama wengi walivyozoea, kuliko kujaribu makubwa na kuanza kuwafanya watu wamshangae. Na pia wanaogopa wakijaribu makubwa na kushindwa, watu watawacheka na kuwasema vibaya.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Changamoto Za Kuondoka Kwenye Vifungo Vya Maisha Na Kupata Uhuru Wa Maisha.
Unaondokaje kwenye utumwa huu wa kujinunulia?
Siyo rahisi kama unavyofikiri kwamba KUANZIA SASA SIJALI TENA WATU WANAFIKIRIA NINI KUHUSU MIMI, kwa sababu utaendelea kujali, kama hutaaniza kwenye mzizi wa tatizo hili.
Mzizi wa tatizo hili ni kutokujua kusudi la maisha yako, kutokujua mambo unayosimamia kwenye maisha, na hivyo kuyumbishwa na mawazo ya kila mtu. Pia hofu imekuwa inawafanya wengi kuendelea kuwa watumwa.
Hatua ya kwanza; jua kusudi la maisha yako, upo hapa duniani kufanya nini.
Hatua ya pili; jua ni vitu gani unavyosimamia, ni maadili gani muhimu kwako.
Hatua ya tatu; jua watu ambao watanufaika na kile unachokwenda kufanya, hawa ndiyo watakaokusukuma kwenda mbele zaidi.
Hatua ya nne; weka malengo na mipango ya maisha yako, muda mfupi na muda mrefu.
Hatua ya tano; chukua hatua, FANYA, FANYA, FANYA. Ukishindwa jifunze na boresha zaidi, usikate tamaa mpaka pale umepata ulichokuwa unataka.
Fanyia kazi haya rafiki yangu, ili ununue uhuru wa maisha yako. kumbuka hakuna mafanikio kama hakuna uhuru.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)