Unataka kila mtu akupende?

Unataka kila mtu akukubali kwa kile unachofanya?

Unataka kila mtu akubaliane na wewe na kukusifia kwenye kile unachofanya?

Basi nina jibu rahisi kwako, ondoka kwenye hii dunia. Kwa sababu unachotaka hakipo, na pia hakiwezi kutokea kwenye dunia hii. Huwezi kupendwa na kila mtu, huwezi kukubalika na kila mtu, hata kama ungekuwa mtu mwema kiasi gani.

Kuna watu ambao watakukubali na kukusifia hata kama utafanya jambo la kijinga kiasi gani. Pia kuna watu ambao watakupinga na kukukataa hata kama unafanya jambo jema kiasi gani. Unachotakiwa kujua ni kipi unasimamia wewe, na endelea kukisimamia, wale wanaokuelewa mtakwenda pamoja, na wale wasiokuelewa wataendelea na mambo yao.

Usijaribu kupoteza hata sekunde moja ya maisha yako kujaribu kumridhisha na kumfurahisha kila mtu, hii ni njia rahisi sana kwako kushindwa. Utaacha yale ambayo ni ya muhimu kwako ili kuwapatia watu kile wanataka, wakati huo kuna wengine unawaangusha.

Wafanyabiashara tunapaswa kulielewa hili vizuri sana, kwa sababu siyo kila mtu anaweza kuwa mteja wako. Kuna watu wanaweza kukuambia hatununui kwako kwa sababu unauza ghali sana, lakini watu hao hata ukiwauzia kwa bei ndogo kabisa inayokupa wewe hasara hawatakosa kingine cha kulalamikia. Hivyo badala ya kutafuta njia ya kukubalika na kila mtu, ni vyema kujiweka kwa namna ambayo wale ambao ni sahihi kwako watavutiwa na wewe na mtafanya biashara pamoja.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Changamoto Za Kuondoka Kwenye Vifungo Vya Maisha Na Kupata Uhuru Wa Maisha.

Kwenye kazi pia tunapaswa kulielewa hili vizuri, kwa sababu watu wengi wamekuwa wanapata shida kwenye kazi zao kwa kushindwa kuelewa wafanye nini. Kwa sababu kila wanachofanya wanapata upinzani kutoka kwa wengine. Unahitaji kuchagua kitu kimoja ambacho unaweza kukisimamia na komaa nacho, wale wa kukuelewa watakuelewa vizuri sana.

Huwezi kuwa kila kitu kwa kila mtu, na wala usijaribu kufanya hivyo. Jua unasimamia nini, kisimamie kweli kweli na utapata wale wanaokuelewa, ambao mtakwenda pamoja.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)