Sifa yako ni vile ambavyo watu wengine wanakuchukulia wewe. Hii inatokana na vile unavyofanya mambo yako na unavyowafanyia wengine. Maneno pekee hayakujengei sifa, bali matendo yako.

Watu wanaamua wakuchukulieje kulingana na unavyoathiri na kugusa maisha yao. Siyo wewe unayeamua watu wakuchukulieje, bali ni wao wenyewe. Japo huna nguvu ya kuwaambia watu wakuchukulieje, unaweza kujijengea njia ambayo itawafanya watu wakuchukulie vile unavyotaka wewe.

Katika kipindi chote cha maisha yako, utajulikana kama mtu ambaye anatatua matatizo ya wengine au mtu ambaye anawatengenezea wengine matatizo. Yote haya yanatokana na jinsi unavyowatendea wengine.

Leo nakushirikisha njia nne za kujijengea sifa yako;

  1. Fanya kile ambacho umesema utafanya, tekeleza kila unachoahidi, maliza kila unachoanza na tekeleza majukumu yako kwa wakati. Unapoishi maneno yako unajijengea sifa ya uaminifu na umakini kwa wengine. Tekeleza kile ulichoahidi hata kama itakuchukua gharama kubwa kuliko ulivyotegemea, ni sifa yako unatengeneza, kuwa tayari kulipa gharama.
  2. Fanya kazi iliyo bora, chochote unachokubali kufanya, kifanye kwa ubora wa hali ya juu, usiguse juu juu na kuacha, labda kwa sababu unalipwa kidogo. Fanya kazi iliyo bora au usifanye kabisa. Kwa sababu kazi yako itaonekana na wengi na watajenga sifa yako kutokana na kazi hiyo. Kama unafanya kazi ya hovyo watu watakuchukulia siyo mtu makini.
  3. Tengeneza urafiki bora na watu wenye sifa nzuri. Unajulikana kupitia marafiki zako, sifa za marafiki zako utapewa wewe hata kama huna sifa hizo. Hivyo angalia sana ni marafiki wa aina gani ambao unao, wanatoa ujumbe kwa wengine kwamba wewe ni mtu wa aina gani, na watu watakuchukulia kama marafiki zako walivyo.
  4. Usiuze au kusifia kitu ambacho wewe binafsi hutumii. Chochote unachofanya, au kuuza, au kusifia, basi hakikisha wewe mwenyewe upo tayari kukitumia, au unaweza kumruhusu mtu unayempenda mno akitumie. Tofauti na hapo utakuwa unatoa ujumbe kwa watu kwamba hujali kuhusu wao, bali unataka kupata kile unachotaka wewe tu. Kama wewe huwezi kuvuta sigara usimuuzie mtu sigara, haijalishi ni biashara inayolipa kiasi gani, usifanye.

Linda sana sifa yako, inaamua ni vitu gani upate kwenye maisha yako. Sifa yako ina mchango mkubwa sana kwa hapo ulipofika sasa, iwe umefanikiwa au la. Na ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuwa na sifa nzuri, itakayowavutia wale watu ambao watakusaidia kufanikiwa.

SOMA; HEKIMA; Maana Yake, Faida Zake Na Mambo 11 Ya Kufanya Ili Uwe Na Hekima.

Jijengee sifa ya HEKIMA na UADILIFU na utaweza kufikia mafanikio makubwa mno. Hakuna jambo linalomshinda mtu mwenye HEKIMA, na hakuna mtu asiyependa kushirikiana na mtu MWADILIFU.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)