Kuanzisha biashara hakujawahi kuwa zoezi gumu, japo wengi huwa wanafikiria hivi. Huwa wanaona ni vigumu sana kuanzisha biashara kwa sababu wamekuwa anaangalia ni kipi wanakosa. Kwa kuangalia wanachokosa wanashindwa kutumia kile walichonacho kwa wakati huo. Mtu yeyote kwa kutumia mazingira na hali aliyonayo, anaweza kuanzisha biashara yake, kubwa au hata ndogo. Kuanzisha biashara siyo kugumu.
Ugumu kwenye biashara ni kuiendesha na kuikuza. Angalia hapo ulipo na angalia biashara ngapi umezijua kwa zaidi ya miaka 5 iliyopita. Nyingi utaziona zipo vile vile na kuna ambazo zitakuwa zimekufa kabisa. Biashara nyingi huanza kwa hamasa kubwa na watu wanakuwa wamejipanga kuzifanya zifanikiwe. Lakini changamoto zinapobisha hodi ndipo watu wanaelewa ugumu wa kuendesha biashara.
Ugumu mkubwa wa biashara upo maeneo mawili;
Eneo la kwanza ni usimamizi mzuri wa biashara hiyo. Mara nyingi watu wanapoanza biashara huwa hawafikirii sana kuhusu usimamizi, na hakuna kitu kinaua biashara nyingi kama usimamizi mbovu. Biashara inapokosa usimamizi mzuri kutoka kwa mmiliki wa biashara hiyo, hasa mwanzoni mwa biashara, ina nafasi kubwa sana ya kushindwa.
Eneo la pili ni kuikuza biashara hiyo. Hapa ndipo wengi wanakwama, biashara inaweza kuwa inaenda vizuri lakini haipigi hatua, ipo pale pale. Na wengi wamekuwa wanajisahau hasa pale ambapo biashara inamtimizia mahitaji yake kwa wakati huo. Anakuja kustuka pale mambo yanapobadilika, mara nyingi kunakuwa na mtu mwingine ameanzisha biashara inayofanana na hiyo.
Haya ni maeneo mawili makubwa, bado zipo changamoto ndogo ndogo za kila siku ambazo zinakwamisha na kuua biashara nyingi. Hivyo unavyoendesha biashara yako, jua haya na yafanyie kazi. Usikate tamaa au kukimbia pale unapokutana na changamoto.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK