Habari rafiki?
Karibu kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia malengo ya maisha yetu. Kupitia makala hizi za ushauri tunapeana maarifa na mbinu za kuweza kufikia malengo na mipango ya maisha yetu licha ya changamoto tunazokutana nazo kila siku. na kama tunavyojua, changamoto ni sehemu ya maisha yetu.

Leo tunakwenda kushauriana kuhusu wateja wa biashara. Watu wengi wanapofunga au kupanga kufungua biashara, huwekeza muda mwingi kufikiria wazo la biashara na mtaji wa kuanza biashara hiyo. Lakini yapo maeneo mengine mengi ya biashara ambayo watu wamekuwa hawayafikirii wakati wanaanza. Hili hudhihirika pale biashara inapoanza na changamoto kuanza kuonekana.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.


Watu wengi wamekuwa wanafikiria kwamba ukishakuwa na biashara basi wateja watajaa kwenye biashara yako kununua. Hivyo wanachotafuta ni kuwa eneo zuri ili waonekane na wateja wa biashara hiyo. Mbinu hii ilifanya kazi zamani, ambapo wafanyabiashara walikuwa wachache. Kwa sasa watu wanaofanya biashara kama yako ni wengi, hivyo kutumia mbinu ya wakipita wanione, hutafanikiwa kwa sababu kabla hawajafika kwako wameshawaona wengine wengi kama wewe. Hivyo kama kigezo chao cha kununua ni kuona pekee, atanunua kwingine na siyo kwako.
Ipo njia ya kuwafanya wateja waje kununua kwako hata kama kuna wafanyabiashara wengine ambao ni wa karibu zaidi kwa mteja wako. Njia hii ndiyo tutajifunza kwenye makala yetu ya leo. Kabla hatujaingia kwenye njia hiyo, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu;

Ninatoa huduma ya Secretarial kama biashara, ninavitendea kazi vya kutosha lakini wateja nilio nao ambao ni wakudumu wanapenda sana kukopa na hawalipi kwa muda wengine kutolipa kabisa. Kuna nyakati wateja wanachanganyia wakati mwingine nafungua nafunga hakuna kabisa mteja au unapata 2,000/ 1,000/ 200 au hakuna kabisa na nina miaka 5 sasa kasoro tangu nianze kutoa huduma hii. Nifanyeje sasa ili kukuza huduma yangu hii? Rose P. M.

Kama ambavyo tumesoma maoni ya msomaji mwenzetu hapo juu, changamoto yake kubwa ni hiyo ya kukosa wateja wa biashara yake. Na kama umesoma vizuri utaona anachofanya yeye ni kukaa eneo lake la biashara na kusubiri wateja, mbinu ambayo kwa sasa imepitwa na wakati.
Leo tunakwenda kujifunza upande wa pili wa wateja wa biashara yako. Kama changamoto yako kwa sasa ni wateja hawaji kwenye biashara yako, basi unachokwenda kufanya ni wewe kwenda kule ambapo wateja wapo. Inaonekana ni mbinu rahisi lakini utekelezaji wake ndiyo changamoto. Tutajifunza hapa jinsi ya kuweza kuwafikia wateja wako kule walipo.

SOMA; Mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS. (Njia 85 za kutangaza biashara yako)

Unajuaje wateja wako walipo?
Hii ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya kuwafikia wateja wako, ni lazima ujue kule walipo. Na ili kujua walipo, kwanza lazima ujue wateja wa biashara yako ni watu wa aina gani, ukishawatambua vizuri wateja wako, ndiyo unaweza kuwafikia kule walipo.

Kwa biashara ya ‘stationary’ wateja ni wale watu ambao wanahitaji huduma za uchapaji, huduma za madaftari pamoja na kutengenezewa vitu mbalimbali vya maandishi. Hivyo hapa wateja wanaanzia kwenye maeneo yanayohusika na elimu, kuanzia walimu mpaka wanafunzi. Pia kunahusika na ofisi mbalimbali na hata watu wenye shughuli ambazo zitahitaji huduma ya uandishi. Mfani mtu mwenye sherehe ambaye anataka kuandaa kadi za kuwaalika watu kwenye sherehe hiyo.

Unawafikiaje wateja wako kule walipo?
Hapa kuna njia tofauti za kuwafikia wateja wako,
Kwanza wateja wako wanatakiwa kuwa na taarifa zako kwamba wewe upo na huduma gani unazotoa. Kwa sababu wateja wako wanapopata picha, kitu cha kwanza wanachofikiria ni nani anayeweza kuwatatulia shida hiyo. Hivyo wanapokuwa na taarifa zako, wanaanza kukufikiria wewe na kisha kuja kwenye biashara yako.

Hapa unahitaji kuhakikisha kila mtu ambaye anaweza kuwa mteja wako, basi anajua kwamba upo. Hivyo unahitaji kuwa na njia nzuri ya kuwafikishia wateja wa biashara yako taarifa zako kuhusu biashara unayofanya.
Hapa unaweza kuandaa vipeperushi ambavyo utawapa watu vinavyoeleza kuhusu biashara yako. Unaweza kia kuandaa matangazo mbalimbali ambayo yatawafanya watu wajue ulipo.

SOMA; Ijue sababu hii kubwa iliyopo nyuma ya biashara yako itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Kwa biashara ya stationary kama ya msomaji mwenzetu Rose, unaweza kuandaa vipeperushi vyako na kuvipeleka kula maeneo ambapo wateja wako wanapatikana. Unaweza usiwafikie wote, lakini wale utakaowapata, watakuwa na taarifa za biashara yako.
Njia ya pili ni kwenda moja kwa moja kwa wateja wako na kuongea nao ili kuwapatia bidhaa au huduma unazotoa. Hapa unakutana na wateja na kuwashawishi kwa nini wanunue kwako, au kwa nini wafanye biashara na wewe.

Kwenye biashara ya stationary, unaweza kutembelea mashule na kuongea na walimu ili kuwapelekea zile huduma ambazo wanazihitaji. Mfano labda wanahitaji kupelekewa chaki, au wanahitaji kuchapiwa vitu mbalimbali. unaweza pia kuwapa punguzo maalumu ili waweze kushawishika kufanya kazi na wewe. Kwa kila mtu ambaye unaona anaweza kunufaika na biashara yako, usiache kuongea naye. Kuliko ukae kwenye biashara yako na upate elfu moja kwa siku, ni vyema ukapanga kuongea na wateja hata 10 kila siku, hutakosa wawili mpaka watatu watakaonunua kitu kwako.

Jambo muhimu la kuzingatia unapowafuata wateja kule walipo.
Toa huduma bora sana, mteja anaweza kukubali unapomwambia, lakini lengo lake ni kutaka kujaribu kama kweli huduma zako ni bora. Sasa wewe hutaki kuikosa nafasi hii nzuri sana na ya kipekee. Hakikisha mteja anaposema anajaribu basi anapata kile ambacho hajawahi kupata kwa wengine. Kumbuka mteja wako kwa sasa kuna maeneo mengine ambapo anapata huduma zake. Sasa anapojaribu yako, ni lazima uwe na sababu ya kumtoa kule alipo sasa na kumfanya awe mteja wako wa kudumu.
Hivyo mpe huduma bora sana, mtimizie kile anachohitaji na usiishie hapo pekee, bali nenda hatua ya ziada. Mfanye mteja afurahie kufanya kazi na wewe na awe tayari kurudi tena na kuwaambia wengine pia.

Nimalize kwa kusema biashara siyo kuwa na eneo zuri, wazo zuri na mtaji wa kuanza. Biashara n kitu ambacho kina vitu vingi vinavyoathiri. Ni lazima uweke juhudi kwenye kila eneo la biashara yako. Kama unaona wateja hawaji kwenye biashara yako, basi wafuate kule walipo. Na ukishawapata, wape huduma bora sana ili waendelee kuwa wateja wako wa kudumu.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz  

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.