Kuna baadhi ya mambo huwa tunayasubiria sana kwenye maisha, tukiamini kwamba tukishayapata basi tutakuwa na maisha ya furaha. Inawezekana ni kumaliza masomo, au kupata kazi au kuanzisha biashara. Tunakuwa tunasubiri kwa shauku kubwa sana, na kuamini baada ya hapo tutakuwa na furaha. Tunapata hicho tulichokuwa tunasubiri, lakini cha kushangaza furaha tunakuwa nayo kwa muda mfupi, baada ya hapo tunarudi kwenye hali yetu ya mwanzo.
Tunajua kwamba furaha ya kweli inatoka ndani ya mtu, na siyo nje ya mtu. Lakini pia hata ile ambayo inatoka ndani yetu, mfano tumekamilisha kitu muhimu tulichokuwa tunafanya, nayo imekuwa haidumu kwa muda mrefu.
Hii yote imekuwa inasababishwa na kutokutosheka, au kutokuridhika na kile ambacho tunakipata. Pale tunapopata kile tunachotaka, macho yetu yanafunguka na kuona kumbe kuna zaidi ya tulichokuwa tunatafuta, na hivyo kudharau kile ambacho tumepata kwa sasa na kuangalia kile ambacho ni kikubwa zaidi.
Kwa mfano umeanza masomo ya shahada na ukawa na shauku ya kupata shahada yako, lakini baada ya kumaliza masomo hayo ya shahada unagundua kuna shahada ya uzamili na uzamivu pia. Hapo ndiyo unaona bado hujafanya kazi yoyote kwenye swala la elimu.
Tabia ya kutokutosheka na kile ambacho mtu amepata ni sumu kubwa sana kwenye furaha ya mtu. Siyo vibaya kutaka kupata zaidi, lakini wakati unataka zaidi, usidharau kile ambacho unacho kwa sasa. Thamini kile ambacho tayari umeshapata, ona mchango wake na ridhika nacho. Halafu jipange kupata zaidi ili kuwa bora zaidi.
Yaani ni hivi sababu ya wewe kutoka hapo ulipo na kwenda mbele zaidi siyo kwa sababu pale ulipo ni kubaya kwako, ila kwa sababu unajua na unataka kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa. Kwa mtazamo huu utaanzia hapo ulipo kwa furaha, na hata kule utakapofika utakuwa na furaha, ya kudumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK