Maisha ni kuchagua, upo hapo ulipo leo kutokana na mambo uliyochagua siku za nyuma. Na mambo utakayochagua leo, yataathiri maisha yako ya siku zijazo.
Moja ya mambo tunayochagua kila siku ni kile tunachofanya kwenye maisha yetu. Kile ambacho tunaweka ujuzi, muda na nguvu zetu, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla.
Sasa unaweza kuchagua kufanya mambo machache na ukayafanya kwa ubora sana, au unaweza kuchagua kufanya mambo mengi na ukayafanya kwa hovyo.
Kufanya machache.
Unapochagua kufanya machache, maana yake unazipeleka nguvu zako kwenye hayo machache muhimu. Unatumia vizuri muda na ujuzi wako kuhakikisha unapata matokeo bora. Unapofanya machache maana yake unazikusanya nguvu zako kwenye sehemu moja na nguvu zilizokusanywa ni hatari sana, zinaweza kufanya makubwa.
Kufanya mengi.
Unapochagua kufanya mengi, maana yake unazitawanya nguvu zako kwenye mambo mengi, na mengi kati ya hayo siyo muhimu. Unaugawa muda mdogo ulionao kwenye vitu vingi unavyofanya na mara nyingi unakuwa huna ujuzi na utaalamu wa kutosha kwenye kila kitu. Kinachotokea ni kutoa matokeo mabovu sana kwenye hayo mengi unayofanya.
Kwa kuwa nguvu na muda wetu una kikomo, tunapojaribu kufanya mengi tunazidi kufikia ukomo wetu na hivyo kushindwa kupata matokeo bora.
Ufanye nini?
Orodhesha mambo yote ambayo unafanya, orodhesha yote kabisa.
Kisha yapange kwa umuhimu, lile muhimu kabisa lipe namba moja, linalofuatia namba mbili na kuendelea mpaka la mwisho.
Baada ya kuyapa namba kwa umuhimu, yaorodheshe tena kwa kuanza na namba moja mpaka ya mwisho. Kisha chora mstari kwenye namba tano, na fanya hayo ya juu yaani moja mpaka tano. Hayo ya chini wala usiyaangalie tena.
Ukifanya hayo muhimu zaidi, hayo mengine yatakuwa sawa yenyewe. Kazana na yale machache muhimu zaidi kwako. Hayo ndiyo yatakuletea matokeo bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK