Kuna tabia mbili muhimu sana kila mjasiriamali anapaswa kujijengea. Hizi siyo tabia za kuzaliwa nazo, bali kila mtu anajijengea kadiri anavyokwenda na maisha yake. Kwa tabia hizi mbili, mtu ataweza kufanikiwa kupitia ujasiriamali.

Tabia ya kwanza ni KUJUA WAKATI GANI WA KUCHUKUA HATARI.

Maamuzi mengi kwenye ujasiriamali ni maamuzi ambayo kwa fikra za kawaida ni hatari. Kwa sababu wajasiriamali tunafanya vitu ambavyo hatuna uhakika navyo, vitu ambavyo havijawahi kufanywa huko nyuma au kwa pale tulipo.

Imekuwa ni dhana ya kawaida kwamba mjasiriamali lazima uchukue ‘risk’. Lakini siyo kila risk inakufaa kuchukua, kuna risk unazichukua na zinakuwa na manufaa kwako, zipo ambazo unachukua na zinakupoteza kabisa.

Wewe kama mjasiriamali unahitaji kujijengea tabia ya kukuwezesha kujua risk gani inakufaa wewe kuchukua na ipi uachane nayo.

Tabia hii unajitengenezea kwa uzoefu kadiri unavyokwenda. Nikuambie wazi kabisa, hakuna shule au darasa lolote ambapo utaweza kufundishwa tabia hii. Utajifunza kutokana na makosa ambayo unayafanya na hivyo kujua ni risk zipi zinakufaa na zipi hazikufai.

Jijengee tabia hii kwa kuangalia kila hatua ambazo umewahi kuchukua, zipi zimekuwa na manufaa na zipi hazijawa na manufaa.

Tabia ya pili ni JINSI YA KUFANYA MAAMUZI.

Hakuna kitu ambacho ni changamoto kama kufanya maamuzi kwenye ujasiriamali. Changamoto hii kubwa inatokana na ukweli kwamba kwenye ujasiriamali mara nyingi utahitaji kufanya maamuzi kabla hata hujawa na taarifa za kutosha. Wakati mwingi unahitaji kufanya maamuzi ya haraka ili usikose fursa fulani. Na hapa ndipo wengi huwa wanafanya maamuzi mabovu na yanawagharimu.

Unahitaji kujijengea tabia ya kuweza kufanya maamuzi sahihi kwa kile ambacho unafanya, maamuzi ambayo yatakuwa na tija hata kama hujapata taarifa za kutosha.

Hii nayo pia ni tabia unayojijengea kadiri unavyokwenda, hakuna mtu atakufundisha hili, bali utajifunza kutokana na maamuzi unayofanya kila siku.

Jijengee tabia hizi mbili muhimu kwenye ujasiriamali, kwa sababu kuchukua risk ni sehemu ya ujasiriamali, lakini lazima uchukue risk za akili. Pia unahitaji kufanya maamuzi bora hata kama hujapata taarifa za kutosha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK