Asubuhi njema rafiki yangu.
Hongera kwa siku hii mpya ya leo, ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile tunachofanya. Tutumie muda wa leo vizuri rafiki.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu PONZI SCHEME,
Ponzi scheme au kwa kiswahili mchezo wa upatu, ni utapeli wa kifedha ambapo mtu anaanzisha mfumo wa biashara ambao unawanufaisha wachache na baadaye kuja kuwaumiza wengi.

Kupitia mfumo huu, mtu anakusanya hela za wengi, na kuwapa wachache sehemu ya hela hizo. Mwanzoni mwa mfumo huu huwa unaonekana ni mzuri sana, huwa unaonekana ni mkombozi.
Lakini kadiri unavyokuwa ndivyo unavyoonesha utapeli wake.

Mfano wa ponzi scheme ni pale unapoambiwa jiunge kwa kutoa elfu kumi, halafu waunganishe watu watano ambao nao watatoa elfu kumi kumi, na wewe utapewa elfu 50.
Kwa hesabu za haraka hii ni rahisi, na tamu pia, natoa elfu kumi, napata elfu 50.
Changamoto inakuja kwamba ili wale watano nao wapate elfu 50 kama wewe, inabidi kila mmoja naye atafute watu watano wa kutoa elfu 10 kila mmoja, hivyo kwa sasa mnakuwa watu 5 x 5 ambayo ni sawa na 25.
Sasa mfumo huu unaendelea kukua, changamoto inakuja pale ambapo namba ya watu imeshakuwa kubwa sana kiasi kwamba hawapatikani wengine wa kujiunga, hivyo wale wa mwisho kujiunga wanakuwa ‘wameliwa’.
Epuka sana mifumo ya aina hii.
Utaijuaje mifumo hii?
1. Kama inaonesha kupata hela ni rahisi, huhitaji kufanya kazi yoyote kimbia.
2. Kama kama hakuna thamani yoyote inayozalishwa au kuzungishwa kimbia.
3. Kama msisistizo ni utatajirika haraka bila ya kuuza chochote au kutokwa jasho kwa njia yoyote kimbia.

NENO LA MWISHO;
Shughuli ya kutafuta fedha kihalali haijawahi kuwa nyepesi, hivyo jiandae kuweka juhudi na kutoa thamani kwa wengine, upate fedha kihalali, au hangaika na mifumo ya uongo na upoteze muda wako, na fedha usipate.
Maisha ni yalo, uchaguzi ni wako.

Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info

img_20161027_071957