Habari za asubuhi rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NGUVU tunayohitaji ili kuleta mabadiliko kwenye maisha yetu.
Wote tunajua ya kwamba kama tunaendelea kufanya yale tunayofanya, tutaendelea kupata matokeo tunayopata na tutakuwa hapa tulipo sasa.

Tunajua ya kwamba ili kupiga hatua zaidi ya hapa tulipo, nguvu inahitajika. Nguvu inahitajika ili tutoke hapa tulipo sasa, na kuweza kwenda mbele zaidi. Na hapa kwenye nguvu ndipo wengi wanapochelewa.
Wengi wamekuwa wanafikiri kwamba hawana nguvu ya kuleta mabadiliko hayo kwenye maisha yao.
Wengi wamekuwa wanasubiri mpaka wengine wawape nguvu hizo, au wachukue hatua ili kuwasukuma.

Ukweli ni kwamba, hakuna nguvu yoyote ya nje inayoweza kukutoa hapo ulipo sasa. Nguvu ya kufanya mabadiliko tayari ipo ndani yako. Nguvu hiyo imetulia, haiwezi kufanya kazi mpaka wewe ufanye kazi kwanza.
Nguvu hii haiwezi kuleta mabadiliko kwenye maisha yako kama huwezi kuitumia.
Nguvu hii ni sawa na gari, kama gari ina gia tano, na wewe umekuwa unatumia gia moja pekee, huwezi kuona nguvu yote ya gari hilo. Ili kuona nguvu halisi, ni lazima utumie gia zote.
Hivyo pia kwako binafsi, huwezi kuona nguvu yako halisi kama hujachukua hatua na kutumia nguvu hiyo.

Anza sasa kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yako. Ufanye makubwa na kupata mafanikio.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info

img_20161027_071957