Maisha yetu hayapo sawa muda wote, siyo kila wakati utakuwa kwenye hisia zako bora kabisa. Kuna wakati utakuwa umekasirishwa, kuna wakati utakuwa umekatishwa tamaa, na upo wakati ambao utakuwa hujisikii tu vizuri. Sisi ni watu na hisia zetu zinabadilika kulingana na kile tunachopitia kwa wakati fulani.
Pamoja na haya yote, lakini bado una jukumu kubwa kwa mteja wako kila siku, jukumu la kumpa kilicho bora. Jukumu la kumpa mteja wako kilicho bora, linaanza na kuvaa tabasamu muda wote, bila ya kujali unapitia nini. Muda wote unaokuwa kwenye biashara yako, au eneo lako la kazi, hakikisha unavaa tabasamu, hii ni hatua ya kwanza kabisa ya kumpa mteja wako kilicho bora.
Usiruhusu mabadiliko yako ya kihisia yaingilie biashara yako au kazi yako. Usitoke na hasira zako ukaja kuzileta kwa wateja wako. Na hata kama umeamka na ugomvi nyumbani kwako, ukishafika kwenye kazi au biashara yako, weka hayo pembeni, vaa tabasamu kwenye uso wako na mpe mteja wako huduma bora kabisa.
Mteja hataki kujua wewe una hisia gani kwa wakati fulani, yeye atakachohukumu ni kama amepata huduma bora au la, na baada ya hapo ataamua kama aje tena au asije tena. Na kumbuka haiishii hapo, atawaambia wengine pia kama waje au wasije. Ni muhimu sana kuzingatia hili, hisia zako mbaya za siku moja, zinaweza kukupoteze wateja milele.
Mara zote mpe mteja wako kilicho bora, hata kama una siku mbaya kwa siku hiyo, acha hayo nyuma na mwangalie mteja wako.
Kwa nini kuvaa tabasamu ni hatua ya kwanza ya kumpa mteja huduma bora?
- Kutabasamu kunaonesha una furaha, watu wenye furaha wanawavutia wengine kuwa karibu nao. Tabasamu mara zote kwenye biashara yako au kazi yako, utawafanya watu kujisikia salama kuwa kwako.
- Kutabasamu kunaonesha kujiamini, na watu wanapenda watu ambao wanajiamini. Unapotabasamu unatoa picha kwamba unajiamini kwa kile unachofanya, na watu watakuwa tayari kupata kutoka kwako.
Mabadiliko yako ya kihisia, yasiiingilie kazi yako au biashara yako, kama huwezi kujizuia ni vyema usiende eneo la kazi au biashara mpaka pale utakapokuwa umekaa sawa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK