Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi zaidi kwenye kile ambacho unafanya.
Rafiki, tumia nafasi ya leo vizuri, huwezi kuipata tena kwenye maisha yako.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhush KUACHA KUCHIMBA…
Ukishagundua tayari upo kwenye shimo, hatua ya kwanza ni kuacha kuchimba,
ACHA KUCHIMBA RAFIKI, acha kabisa, hiyo ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya kuondoka kwenye shimo.
Kama tayari upo kwenye madeni, acha kukopa, acha mara moja.
Kama tayari upo kwenye migogoro na ugomvi na wengine, acha kutengeneza migogoro hiyo.
Kama tayari upo kwenye umasikini, acha kufuga umasikini huo.
Kama tayari afya yako ni mbovu, acha kufanya yale yanayoharibu afya yako, ulevi, uzembe…
Rafiki, ni lazima uchukue hatua haraka sana ya kuacha kile ambacho kinakuweka kwenye hali ambayo huipendi. Hii ni hatua ya kwanza kabisa ya kufika kule unakotaka kufika.
Angalia njia mbadala za kukufikisha pale unapotaka kufika, ila kwanza acha zile njia zinazokupoteza. Kutafuta njia sahihi kwa kuendelea na njia inayokupoteza ni kujidanganya, huwezi kufika popote.
UKISHAGUNDUA UPO KWENYE SHIMO, ACHA KUCHIMBA.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info