Kuna baadhi ya mambo huwa tunajikuta tunayafanya, lakini hatujui ni kwa jinsi gani yanatupotezea muda wetu. Na moja ya mambo hayo ni kubishana. Unajikuta unaona ni sahihi kabisa kwako kubishana, kwa sababu wewe ndiyo uko sahihi na yule mwingine amekosea au  hajui.

Si ndiyo, wewe shabiki wa yangu upo sahihi kuliko yule shabiki wa simba. Au wewe ccm uko sahihi kuliko yule chadema. Au wewe mwislamu upo sahihi kuliko yule mkristo. Na kwa kuwa uko sahihi, lazima umwoneshe yule mwingine kwa nini hayupo sahihi. Basi unatumia nguvu zako kuhakikisha umemwonesha.

Utatumia nguvu zako zote, utafungua mpaka vifungu vya maandiko kudhibitisha kile unachotaka kudhibitisha, lakini unajua nini, umepoteza muda kwao. Kwa sababu, sijawahi kuona au kusikia mtu amebadili mawazo yake au maamuzi yake baada ya mabishano. Kibaya zaidi ni kwamba, kadiri unavyozidi kubishana ndivyo unavyozidi kumpa mtu nafasi ya kuamini kile anachoamini.

Kubishana ni kupoteza muda wako kwa sababu kwa kubishana unakuwa unaamini kwamba unaweza kutumia nguvu kuwabadili watu. Kitu ambacho unakuwa hujajua ni kwamba kwa asili watu wanapenda kupinga nguvu yoyote inayotaka kuwabadili. Hivyo unapobishana na mtu kuhusu kitu fulani, humsogezi hata karibu aanze kufikiria kile unachofikiria, badala yake unamfukuza zaidi, unamfanya azidi kuwa mbali na pale unapotaka awe yeye.

Ufanye nini?

Kwa kuwa watu hawawezi kubadilika kwa njia ya mabishano je tuwaache watu waende wanavyotaka hata kama hawajaujua ukweli? Hapana, ipo njia bora ya wewe kuwawezesha watu kuujua ukweli.

Na njia hiyo ni elimu. Badala ya kubishana na watu, wape elimu. Toa elimu ya kile ambacho unajua ni sahihi, na toa kwa njia rahisi kueleweka. Wapo watakaopinga, lakini wewe achana nao, endelea kutoa elimu. Kitakachotokea ni baadhi ya watu wanaopenda ukweli wataanza kuuona kupitia elimu unayotoa, na watakuwa tayari kujifunza na watajibadilisha wao wenyewe.

Njia nyingine ya kuepuka kubishana ni kuonesha kwa vitendo, badala ya kutumia nguvu nyingi kuongea kwenye mabishano, onesha, watu wanaamini zaidi wanapoona kuliko wanaposikia. Unajua kwa nini? Kwa sababu kila mtu anaweza kuonea, ila kufanya, wachache sana wanaoweza.

Hapa unakuwa umetumia nguvu zako kuleta mabadiliko mazuri kwa watu.

Usibishane, fundisha, usilazimishe watu kuamini kile unachoamini, bali wape uelewa bora zaidi. Na wao wenyewe watachagua kuchukua hatua ambayo ni sahihi kwao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK