Katika maisha, kuna makundi mawili makubwa ya watu;

Kuna wamiliki wa vitu, hawa ni wale ambao wanachukua mamlaka makubwa juu ya kitu chochote na kuhakikisha kinakwenda kama wanavyotaka kiende. Watu hawa wanaweka juhudi kubwa kuhakikisha wanatoa matokeo makubwa. Kama kitu chochote hakitokei, wanajua ni kwa sababu kuna juhudi hawajaweka.

Kuna wale wapitaji au watumiaji wa vitu. Hawa hawana umiliki, wao wapo wapo tu, mguu nje mguu ndani, wanagusa tu na kupita. Hawajipi jukumu lolote kwa chochote wanachofanya, wanajua siyo juu yao.

Kundi la kwanza la wamiliki wanafanikiwa sana kwa sababu wanajitoa kuhakikisha chochote wanachogusa kinakuwa bora sana. Kundi la pili wanaishia kuwa watazamaji na watu wa kawaida kwa sababu hawajitoi kuhakikisha mambo yanatokea.

Kama upo kwenye biashara, imiliki biashara yako, jua kila kitu ni jukumu lako na hakikisha unaweka kila juhudi iliyo ndani ya uwezo wako kuhakikisha biashara yako inakua. Kama mambo hayatokei usitafute sababu yoyote ya nje, badala yake angalia ni juhudi zipi huweki, ni wapi unazembea na pabadilishe. Kwa kuimiliki biashara yako, lazima utaona mafanikio makubwa.

Kama upo kwenye ajira, miliki kazi yako. Chochote ambacho umepangiwa kufanya, usichukulie kama kazi ya mtu mwingine, bali chukulia ni kazi yako wewe na unahitaji kutoa matokeo bora zaidi. Japokuwa ni kazi ya mtu mwingine, lakini kiuhalisia ile ni kazi yako, na sifa yoyote nzuri au mbaya unayotoa kupitia kazi hiyo, itaandamana na wewe maisha yako yote.

Miliki maisha yako, miliki mahusiano yako na miliki jamii yako. Miliki muda wako, miliki fedha zako na miliki nguvu zako. Chochote ambacho unahusika nacho, hakikisha unaweza kukitumia vizuri kabisa kupata matokeo bora. Unahitaji kuwa mchezaji hasa na siyo mtazamaji pekee.

Anza kucheza sasa, shika umiliki wa kila kitu unachofanya kwenye maisha yako kwa asilimia 100. Hapa ndipo mafanikio yako yalipo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK