Hongera rafiki yangu kwa siku nyingine nzuri sana ya leo.
Leo ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tunafanya kwenye maisha yetu. Leo ni siku ambayo tunaweza kuweka alama mpya kwenye maisha yetu.

img_20161112_091656

Asubuhi ya leo titafakari kuhusu LEO TENA…
Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba mafanikio ni kitu cha mara moja, kitu ambacho kinakuja kama ajali.
Wengine wanafikiria ni kitu cha kulala masikini na kuamka tajiri. Au kukitana na zali fulani halafu ukapata ulichokuwa unatafuta muda wote.
Huu ni uongo na umewazuia watu wengi kupata kile ambacho wanataka.

Ukweli ni kwamba mafanikio yoyote yanakuja kidogo kidogo. Hatua ndogo ndogo unazopiga kila siku, zina mchango mkubwa sana kwenye maisha yako,
Japo leo unaweza kuona ni hatua ndogo, kadiri unavyorudia kila siku bila ya kukata tamaa, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya mafanikio.

Hivyo rafiki, LEO TENA, nenda kapige hatua ndogo kuelekea kwenye mafanikio yako.
Leo tena nenda kaongeze juhudi kwenye kile unachofanya.
Leo tena nenda kaongeze muda wa kufanya kazi yako.
Leo tena nenda kajaribu kitu kipya, hata kama ni kidogo sana.
Leo tena nenda kakutane na watu wapya ambao mtatengeneza uhusiano kupitia kile unachofanya.
Leo tena nenda kaboreshe mahusiano yako na familia yako na wale wanaokuzunguka.
Leo tena kahakikishe afya yako inakuwa bora kw akichagua vyakula bora na kufanya mazoezi.
Leo tena nenda katenge kiasi kidogo cha kipato chako na kifanye akiba.
Leo tena kaangalie maeneo ambayo unaweza kuwekeza ili siku zijazo uwe na uhuru wa kifedha.

Yote haya ni mambo ya kufanya kila siku, KILA SIKU. Na siyo kufanya kwenye zile siku ambazo unajisikia.
Jifunze kujiwekea nidhamu ya kufanya mambo haya madogo kila siku, na siyo kutaka kuanza na makubwa hapafu ukaishia njiani.

Ni leo tena rafiki, leo tena kapige hatua muhimu ya kuelekea kwenye maisha ya mafanikio.
Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.

Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info