Hongera rafiki kwa asubuhi nyingine nzuri ya leo.
Leo ni siku bora na ya kipekee, ni siku yetu ambapo tunakwenda kufanya makubwa kwenye maisha yetu.
Tutumie nafasi ya leo vizuri rafiki, tuweze kupiga hatua.

img_20161112_091656

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu AMBACHO HUJII…
Inawezekana unakazana kupiga hatua lakini kila mara unakwama, mara nyingi hii inatokana na vitu ambavyo hujui.
Wakati mwingine wala hakuna makosa unayofanya, lakini hupigi hatua, hii inatokana na vitu ambavyo bado hujavijua

Hivyo basi rafiki, kama unaona husongi mbele licha ya juhudi na maarifa unayoweka, hebu kaa chini na jiangalie vizuri. Je kuna kitu ambacho hujui, ambacho kinakurudisha nyuma?
Hebu waangalie wale waliofika pale unapotaka kufika wewe, je kuna vitu wanafanya tofauti na unavyofanya wewe?
Kama ndiyo vijue na jua namna utakavyorekebisha.

Wakati mwingine inawezekana unajua lakini hufanyi tu.
Yaani unajua kabisa kipi unapaswa kufanya, lakini hukifanyi.
Sasa hapo tatizo ni nidhamu.

Usione aibu kusema hujui kitu fulani, hakuna anayejua kila kitu.
Kila siku ni nafasi nyingine kwako kujifunza. Na wanaojifunza ni wale wanaokiri ya kwamba hawajui.
Kubali hujui, kuwa tayari kujifunza na fanyia kazi yale unayojifunza.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info