Mwandishi wa kitabu cha THE TOTAL MONEY MAKEOVER, Dave Ramsey anasema kwamba matatizo ya kifedha, asilimia 80 yanasababishwa na tabia za watu na asilimia 20 yanasababishwa na ukosefu wa walimu na maarifa sahihi ya kifedha.

Hivyo kama una tatizo lolote la kifedha hapo ulipo sasa, kwa sehemu kubwa sana limesababishwa na tabia ambazo tayari umeshajijengea kwenye matumizi yako ya fedha.

Kama ambavyo tunajua, huwa tunajenga tabia sisi wenyewe, lakini baadaye tabia zinatujenga. Wanasema tabia ni kama kamba nyembamba, ambayo kila siku unajizungushia, unapokuja kustuka, unajikuta huwezi kuondoka tena kwenye kamba hiyo.

Sasa zipo tabia ambazo zimekuwa zinakuingiza kwenye matatizo ya kifedha. Na tabia hizi zinatokana na udhaifu ambao mtu unao. Kwanza kubali kwamba una udhaifu kwenye maeneo fulani ya maisha yako. Maana kila mtu ana udhaifu, hivyo unapoujua udhaifu wako unajipanga ili usikuingize kwenye matatizo.

Linapokuja swala la fedha, hebu jiulize wewe ni hatua zipi umekuwa unachukua? Je maisha yako yanabadilika ukiwa na fedha na ukiwa huna fedha? Je watu wa kukuangalia tu kwa nje wanajua leo una fedha au huna fedha? Je siku ukipata fedha unakula na kunywa na siku ukikosa unakaa na kusikitika?

Kama umekuwa unaonesha tabia hizi kifedha, basi una udhaifu mkubwa ambao ni kushindwa kujidhibiti kifedha. Kama mtu kwa kukuona tu anajua una fedha au huna, ina maana unaruhusu fedha iamue maisha yako yaweje, badala ya wewe kuamua hilo.

Moja ya vitu unapaswa kudhibiti kuhusu fedha ni matumizi na hapa kwenye matumizi watu wengi wamekuwa na udhaifu.

Nikuulize swali, je umewahi kwenda sokoni ukisema unaenda kununua kitu fulani, lakini ukarudi nyumbani na vitu vingi kuliko ulivyokuwa unategemea? Kama ni mnywaji, umewahi kwenda bar ukisema utakunywa chupa mbili lakini unakuja kustuka umekunywa zaidi ya tano na kuwanunulia wengine wengi? Je umewahi kutoka nyumbani huna mpango wowote wa kununua nguo lakini ukarudi nyumbani na nguo?

Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote hapo, basi una udhaifu kwenye fedha, huwezi kudhibiti matumizi yako ya fedha na kila siku utajikuta kwenye matatizo ya kifedha.

Ukishajua udhaifu wako wa kifedha, usijaribu kupambana nao, kwa sababu utaufanya uwe imara zaidi. Badala yake ondoka kwenye mazingira yatakayochochea udhaifu wako.

Na moja ya njia za kufanya hivyo ni kubeba kiasi cha fedha kinachotosha kwa kile ambacho unakwenda kufanya. Kama unaenda sokoni, orodhesha kila utakachonunua na bei zake, kisha beba kiasi hicho tu cha fedha. Kama unaenda baa, beba fedha ya chupa ulizopanga kunywa. Kama una udhaifu kwenye fedha, kwa sasa usiwe na fedha ambayo haina matumizi, utajikuta umeshaipatia matumizi, na wakati unaitumia utajiona upo sahihi kabisa, ila baadaye ndiyo utagundua umekosea

Unapopanga kuondokana na udhaifu huu, hakikisha pia huweki mazingira rahisi ya kupata fedha ya haraka pale unapohitaji. Hivyo usitembee na kadi za malipo au kadi za kutoa fedha kwenye mashine za benki. Na Kama unatumia huduma za fedha kwenye mitandao ya simu, pia fanya iwe vigumu kwako kutoa fedha hizo kwa haraka.

Hili ni suluhisho la muda, wakati unaendelea kurekebisha tabia yako na kujijengea nidhamu ya matumizi ya fedha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK