Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa nafasi hii ya kipekee nw nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya kwenye maisha yetu.
Itumie nafasi ya leo vizuri rafiki yangu, haitarudi tena ikishapita.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NYEUPE, NYEUSI NA KIJIVU….
Kuna vitu kwenye maisha yetu ni VYEUPE, yaani moja kwa moja ni kitu sahihi kwetu kufanya, ni faida kwetu kufanya na hatuna wasiwasi wowote. Ni uhakika kufanya mambo haya unafanikiwa.
Kuna vitu kwenye maisha yetu ni VYEUSI, yaani moja kwa moja ni kitu ambacho siyo sahihi kufanya, ni makosa makubwa, ni hasara kubwa kufanya viru hivi. Ni uhakika kwamba ukifanya vitu hivi umechagua wewe mwenyewe kushindwa.
Kuna vitu kwenye maisha yetu ni KIJIVU, yaani siyo vyeupe wala siyo vyeusi, vina weupe na pia vina weusi ndani yake. Hivi ndiyo vitu ambavyo hatuna uhakika kama ni sahihi au siyo sahihi, hatuna uhakika kama tukifanya tutapata faida au hasara. Hivi ndivyo vitu vinavyotuumiza kichwa zaidi.
Sasa changamoto kubwa kwenye maisha yetu zinatokana na vitu hivi ambavyo ni vya KIJIVU, maana hivi ndiyo vimebeba sehemu kubwa ya maisha yetu.
Ni vitu vichache sana ambavyo ni vyeupe au vyeusi kwenye maisha yetu. Vitu vingi vinaangukia kwenye kijivu na hivyo hatuna uhakika wa jambo lolote.
Kila tunalofanya, tuna nafasi ya kufanikiwa na nafasi ya kushindwaa pia. Kuongeza nafasi zetu za kufanikiwa na kuwa na maisha bora, tuongeze uwezo wetu wa kugeuza kijivu kuwa nyeupe. Tuweze kuzitumia changamoto zetu kufanikiwa zaidi.
Jua muda wote upo kwenye GREY ZONE, na usijipe uhakika sana kwa jambo lolote, hata kama ulilifanya jana.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info