Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Ni imani yangu kwamba umeianza siku hii ya leo vizuri sana.
Najua una hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi zaidi kwenye kile ambacho umechagua kufanya. Hongera sana kwa siku hii ya leo rafiki.
Nenda kaulinde sana muda wako, maana hiyo ndiyo rasilimali kuu ya mafanikio yako.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kulipa gharama.
Kila kitu unachotaka kwenye maisha yako, kuna gharama ambayo unapaswa kuilipa. Bila ya kulipa gharama hiyo, hutaweza kupata unachotaka, na kama utakipata basi hakitadumu kwa muda mrefu.
Sasa muhimu zaidi ni hili, gharama unayokuwa tayari kulipa, ndiyo thamani utakayopokea kwenye maisha yako. Kama utalipa gharama ndogo utapokea thamani ndogo, na kama utalipa gharama kubwa utapokea thamani kubwa.
Kwa mfano, ukitaka kutoka Dar kwenda Arusha kwa basi utalipa elfu 30 kama nauli. Lakini kama utatumia ndege utalipa siyo chininya laki tatu. Kuna gharama kubwa kwenye ndege kwa sababu kuna thamani kubwa unayopata kama utatumia ndege, na moja ya thamani hiyo ni muda. Utatumia masaa 10 kwa gari wakati utatumia saa moja kwa ndege.
Hivyo ni muhimu sana kujua ni thamani gani unaitaka kwenye maisha yakp, kujua gharama unayopaswa kulipa na kisha kuilipa.
Kama unataka kufikia uhuru wa kifedha, lazima ulipe gharama ya kufanya kazi zaidi ya wengine, kujibana zaidibya wengine na pia kuishi maisha ya tofauti na wengine. Kama huwezi kulipa gharama hiyo huwezi kufikia uhuru wa kifedha.
Je ni gharama gani unayoenda kulipa leo rafiki yangu?
Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani