Watu wengi wamekuwa wakianzisha biashara, ila pale mapema kabisa wanagundua jambo moja muhimu, hawana wateja wa biashara zao. Wakati wanajipanga kuanza biashara wanaona mafanikio yapo nje nje, wanajua kabisa wakishaanza biashara watapata wateja wengi. Ila wanapoanza biashara, ndipo wanapokutana na ukweli, kwamba biashara zao hazina wateja.
Tatizo la biashara kukosa wateja, linaanzia kwenye mipango ya mtu ya biashara. Pale mtu anaposema mteja wa biashara yake ni mtu yeyote, au mteja wa biashara yake ni kila mtu, hapo ndipo anapokuwa amechagua kukosa wateja wa biashara yake.
Hakuna biashara ambayo inawafaa watu wote, hakuna biashara ambayo ina uwezo wa kumfanya kila mtu awe mteja wake. Ndiyo maana kuna bidhaa na huduma mbalimbali kwenye kila aina ya biashara.
Mteja mgumu kabisa kumpata kwenye biashara ni yeyote au kila mtu. Ukishasema mteja wako ni kila mtu au mtu yeyote, maana yake hujui mteja wa biashara yako ni nani. Unakuwa umechagua kufanya biashara ya kubahatisha, kama mtu ataona aje anunue na kama hatakuja basi.
Mfanyabiashara anajua wateja wa biashara yake ni watu gani, anajua sifa zao na anajua wanapatikana wapi. Muhimu zaidi anajua matatizo na changamoto zao ni zipi na anajua ni namna gani anaweza kuzitatua.
Kwa kujua haya kuhusu mteja wake, mfanyabiashara makini anampa huduma bora na ya kipekee mteja wake na pia anajua atampata wapi. Kama ataanzisha biashara halafu wateja hawapatikani, anajua njia ya kuwafikia au namna ya kuwavutia wateja hao kuja kwenye biashara yake.
Hivyo rafiki, biashara yoyote unayoifanya, chagua aina ya wateja unaotaka kuwahudumia, wajue vizuri kisha wape kile ambacho kitayafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Watu watalalamika kuhusu kukosa wateja ila siyo wewe, kwa kuwa unajua wateja wako ni wapi na wanahitaji nini.
Usifanye biashara ya kubahatisha, chagua wateja wako na wahudumie vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK