Hongera rafiki yangu kwa nafasi nyingine nzuri ya leo.
Hii ni fursa nzuri sana ya kwenda kuweka juhudi zaidi kwenye kile ambacho umechagua kufanya.
Muda wa leo ni wa thamani kubwa sana, utumie vizuri.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu JUSTIFICATION au KUHALALISHA…
Kuna wakati ambapo mtu unafanya jambo na unajua kabisa umekosea kwa kufanya hivyo. Au kuna uzembe fulani unakuwa umesababisha.
Pamoja na kujua kwamba umefanya makosa, unaanza kutafuta sababu kwa nini siyo vibaya sana ulivyofanya, au kwa nini hukuweza kuepuka kufanya hivyo.
Hapo ndipo mtu unakuja na kauli kama..
1. Kila mtu anafanya..
2. Binadamu hatujakamilika…
3. Shetani alinipitia…
Na kauli nyingine kama hizo.
Ninachotaka utafakari asubuhi ya leo rafiki yangu ni hiki,
Kama umefanya makosa, kiri umefanya makosa, yakubali makosa yako na kisha chukua hatua za kufanyia kazi chochote ambacho hakipo sawa.
Usitafute njia yoyote ya kuhalalisha ulichofanya.
Unapokubali makosa au uzembe wako, unakuwa tayari kuchukua hatua na kuyafanya maisha yako kuwa bora.
Nakutakia siku njema njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,