Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu tena kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA, ambapo tunashirikishana misingi muhimu ya kuweza kujenga maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa.
Tupo hapa tulipo sasa kwa sababu sisi ni washindi. Jamii nzima ya binadamu inasonga mbele kupitia ushindani. Kwa sababu mara nyingi rasilimali ni chache kuliko uhitaji, ni sheria ya asili kwamba kumekuwa na ushindani baina ya jamii ya viumbe hai. Kwa mfano kama simba wamekaa porini, wapo labda simba watatu, wote wana njaa, akapita swala mmoja mdogo, yule simba mwenye nguvu na mwenye mwendo wa kasi ndiye atakayefanikiwa kumpata swala yule. Hivyo ushindani baina ya viumbe hai wa jamii moja umekuwepo tangu enzi na enzi, hata miti iliyoota sehemu moja, ule mti ambao ni mkubwa kuliko wenzake ndiyo unafaidi mwanga zaidi, maji zaidi na hata madini zaidi.
Pamoja na kwamba sisi viumbe hai tupo kwenye hali ya kushindana, sisi binadamu tuna uwezo mkubwa kuliko viumbe wengine wote. Tuna utashi ambao umetusaidia kujenga jamii imara zenye ushirikiano wa hali ya juu na hivyo kuweza kuwa salama kwa pamoja kama jamii. Kwa kuweza kuwa ndani ya jamii, tunaweza kuwasaidia wale wanyonge nao kushinda.
Leo tunakwenda kuangalia namna sahihi ya kupima ushindi kwenye maisha. Tutaangalia aina mbili za ushindi ambazo watu wanatumia na mwisho tutaangalia ni aina ili ya ushindi tunapaswa kuitumia sisi wanafalsafa na kuishawishi jamii itumie aina hii ya ushindi ili tuweze kujenga jamii bora na yenye ushirikiano.
Kabla hatujaingia kwenye hizo aina za ushindi hebu tuone mifano michache.
Hebu kumbuka wakati ukiwa shuleni, mme fanya mtihani na ukapewa mtihani wako, kuangalia maksi umepata maksi 33 kati ya maksi 100. Unajisikiaje? Hakika utajisikia vibaya, yaani katika maksi 100 wewe umeweza kupata 33 pekee? Ni dhahiri umeshindwa. Sasa wakati unafikiria maksi zako hizo chache, mwalimu akasema atabandika matokeo ya wote, unaenda kuangalia unakuta nusu ya darasa wamepata maksi chini ya 30, wa kwanza ana maksi 34, waliobaki wana maksi kati ya 30 na 33. Hapa sasa unajisikiaje? Bado utabaki kusikitika kwamba umeshindwa?
Ukweli ni kwamba utapata ahueni fulani, dakika chache zilizopita ulijiona umeshindwa, lakini sasa umeshajua zaidi ya robo tatu ya darasa umewazidi maksi, na mtu mmoja pekee ndiyo amekuzidi maksi. Nafikiri unapata mwanga wa namna tunavyopima ushindi hapo.
Mfano mwingine ni aina ya watu unaokaa nao. Mara nyingi wale watu ambao tunakaa nao muda mrefu, tunafanana nao kwa mambo mengi kwenye maisha. Kipato hamtofautiani sana na hata maisha mnayoishi yanafanana. Sasa pata picha wewe umepiga hatua na wenzako wakabaki pale walipo, au kuna mwingine amepiga hatua na wewe umebaki pale ulipo. Utaanza kujiona kama umepoteza, utajiona umeshindwa. Haiwezekani wenzako wote wana nyumba, wana magari, wana familia ila wewe hujui hata unafanya nini. Lakini mwanzo wote mnapokuwa sawa, hupati shida yoyote.
Kupitia mifano hii miwili, naamini umeanza kupata mwanga ni namna gani tumekuwa tunapima ushindi, kwamba kama mimi nimepata na wengine wamekosa basi nimeshinda. Kama wote tumepata au tumekosa basi mimi siyo mshindi. Hapa ndipo shida kubwa sana za kijamii zinapoanzia, wivu, husda, dhuluma na mengine mengi.
Aina mbili za kushinda.
Zipo aina mbili za kushinda, kulingana na namna watu wanavyochukulia maisha yao.
Aina ya kwanza ni pale mtu anapoona ameshinda kama wengine wameshindwa au wamepoteza.
Hii ndiyo aina ambayo ilikuwa imetawala jamii za zamani. Wengi walifikiri kama hakuna aliyepoteza basi hakuna aliyeshinda. Ndiyo maana hata biashara zilikuwa na ushindani mkali mno. Siku za nyuma, ilikuwa ukianzisha biashara ambayo mwingine anaifanya, yupo tayari kutenga fedha kuhakikisha anakutoa kabisa kwenye biashara hiyo. Ilikuwa ni vita kali mno kibiashara, na wengi waliumia.
Mpaka sasa, watu wengi hujisikia vizuri pale ambapo wao wamepata kitu na wengine wamekosa. Inawafanya waone wao ni wajanja zaidi, au wana uwezo mkubwa zaidi kuliko wengine. Hii ni dhana ambayo inatoa kujisikia vizuri kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu ina madhara.
Madhara ya aina hii ya ushindi ni kwamba inaangamiza jamii nzima, kwa kifupi kila mtu anashindwa. Kama wewe umeshinda, ila wengine wameshindwa, basi wote mmeshindwa. Kwa sababu kushinda kwako hakuna maana kama wengine nao hawanufaiki. Kwa biashara yako kushinda kwa sababu nyingine zimekufa ni kuirudisha jamii nyuma. Kwa sababu kadiri biashara zinavyokuwa nyingi, ndivyo ajira zinavyoongezeka, ubunifu unaongezeka na hata thamani inaongezeka.
Aina ya pili ya ushindi ni kushinda pamoja.
Hapa mtu anaona ameshinda pale tu wengine nao wanapokuwa wameshinda. Kwa sababu wanajua ushindi siyo wa mtu mmoja bali ushindi ni wa jamii nzima. Kwa aina hii ya ushindi mtu hajiangalii yeye mwenyewe bali anamwangalia kila anayehusika.
Aina hii ya ushindi ina manufaa makubwa kwenye jamii, kwa sababu jamii nzima inanufaika pale kila mtu anaposhinda. Kuanzia kwenye kazi, biashara na hata familia, pale kila mtu anaposhinda basi jamii nzima inashinda. Kila mtu anakuwa na furaha, ushirikiano unakuwa mkubwa na kwa pamoja wote mnasonga mbele.
Aina bora ua ushindi kwetu wanafalsafa.
Popote pale ulipo, pima ushindi wako kwa watu wangapi ambao umewawezesha kushinda. Usiangalie ni watu wangapi ambao umeweza kuwashinda, badala yake angalia watu wangapi wanashinda kama wewe. Angalia ni watu wangapi ambao umewawezesha kushinda. Huu ndiyo ushindi halisi kwenye maisha yetu, ambao tunaweza kuufurahia na kujivunia.
Na kama alivyowahi kusema mwandishi ZIG ZIGGLER, unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, kama utawawezesha watu wengi zaidi kupata kile wanachotaka kupata. hivyo ushindi wowote unaotaka kupata kwenye maisha yako, tafuta watu gani utawawezesha kushinda. Wakishinda wao na wewe umeshinda.
Usiogope kwamba wengine wakishinda basi wewe unashuka, hizo ni fikra za kizamani za kuona kuna uhaba wa ushindi hapa duniani. Hata kama rasilimali ni hapa, wote tunaweza kuzitumia vizuri na kila mtu akashinda. Hakuna uhaba wa ushindi hapa duniani, na kadiri watu wengi zaidi wanavyoshinda, ndivyo maisha yanavyozidi kuwa bora zaidi.
Wanafalsafa wote tunapima ushindi wetu kwa kuangalia watu wangapi tumewawezesha kushinda. Kupitia kazi au biashara unayofanya, nenda kawawezeshe watu kushinda, na wewe utashinda pia.
Mwezeshe mtu kushinda kwa kumtumia makala hii kwenye email yake leo, forward email hii kwa marafiki zako ambao ungependa nao washinde kwenye maisha yao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.