Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Hakuna muda mwingine tunaoweza kuutumia zaidi ya leo, jana imepita, kesho bado haijafika.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu urahisi wa kusema na ugumu wa kufanya.
Kusema ni rahisi sana, kila mtu anaweza kusema.
Kupanga ni rahisi sana, kila mtu anaweza kupanga.
Tatizo lipo kwenye kufanya, tatizo lipo kwenye kutekeleza, hapo ndipo changamoto kubwa inapoanzia. Hapo ndipo nidhamu kubwa inapohitajika.
Kwa mfano kila mtu anajua na anaweza kusema kwamba mambo mazuri yanahitaji muda, kwamba mafanikio hayaji haraka. Lakini unapofuatwa na mtu na kuambiwa kuna njia ya haraka ya kutajirika, na akakuonesha watu waliopita njia hiyo, unasahau ule msingi na kujikuta umeshanadaika.
Unajua na ni rahisi kusema kwamba mafanikio yanatokana na juhudi kubwa zilizowekwa kwa muda mrefu kwenye kitu kimoja ulichochagua kufanya. Lakini kila siku unavutiwa na fursa mbalimbali unazoona ni mpya, unahangaika nazo zote na mwisho wa siku unarudi pale pale.
Ni rahisi kusema kwamba utapambana, utang’ang’ana, lakini unapokutana na changamoto unajikuta unaiimbia na kuona huziwezi.
Unahitaji kujijengea nidhamu, ambayo haitayumbishwa na jambo lolote, hata kama litaonekana ni zuri kiasi gani machoni, kama lipo kinyume na msingi, hulifanyi.
Usikazane kusema fanya, kusema ni rahisi, hakuna atakayekushangaaa kwa kusema. Wewe fanya, na matendo yanaongea kwa sauti kuliko maneno.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info