Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya.

img-20161217-wa0002
Tukumbukenya kwamba muda ndiyo rasilimali muhimu sana kwetu, tuutumie muda wetu vizuri.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu HAPO ULIPO SASA,
HAPO ULIPO SASA ndipo unapopaswa kuwa kwa sasa,
Hakuna sehemu nyingine unayohitaji kuwepo kwa sasa, zaidi ya hapo ulipo sasa.
Maana hapo ulipo sasa, ndiyo muda pekee ambao una uhakika nao na unaweza kuutumia vyovyote utakavyo.

Lakini kwa kutokujua, akili zetu zimekuwa zinatudhulumu, zimekuwa zinatutorosha pale tulipo na kutupeleka kule ambapo hatupo.
Hivyo kimwili unakuwa sehemu moja, lakini kiakili upo mbali kabisa.
Kimwili upo kazini, lakini kiakili upo nyumbani.
Au kimwili upo nyumbani lakini kiakili yaani mawazo yako yote na hofu zako zipo kazini.
Sasa unajua nini kinatokea?
Kinachotokea ni kukosa yote, tunakosa pale tulipo sasa na tunakosa kule tu apopafikiria.
Unakuwa kazini na hufanyi kazi kwa ufanisi na wakati huo pia hakuna unachopata kwa akili yako kuwa nyumbani.
Kuepukana na hili na kuweza kutumia muda wako mchache ulionao hapa duniani, kuwa pale ulipo, kwa wakati ambapo upo.
Yapeleke mawazo yako yote kwenye kile unachofanya, iwe ni kazi, mapumziko, kula, kutembea au chochote kile unachofanya.
Jifunze kuyadhibiti mawazo yako na utaona manufaa kwenye chochote kile unachofanya.
Ukiona unasema unapoteza poteza muda, jua akili yako haipo pale ulipo.
Irudishe akili yako pale na yapo mengi mazuri ambayo utayafurahia.

Nakutakia siku njema sana kwako rafiki yangu,
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
#KochaMakirita