Katika maisha yetu ya kila siku, kuna vitu au watu ambao tunawaongoza. Mafanikio yetu katika jambo lolote tunalofanya, yanatokana na uwezo wetu mzuri wa kuongoza.

 

Kila mtu ni kiongozi wake yeye mwenyewe, na wengine wamepata nafasi ya kuwa viongozi wa familia zao, viongozi wa jamii zao, viongozi wa maeneo yao ya kuabudu na hata viongozi wa kitaifa.

Uongozi siyo kitu cha kuzaliwa nacho na wala siyo kitu cha kuzoea. Uongozi una misingi yake na miongozo yake. Marehemu Dr Myles Munroe, alikuwa mwandishi wa vitabu na katika kitabu cha KEYS TO LEADERSHIP anatushirikisha miongozo ya uongozi.
Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia kitabu hiki kizuri.

1. Kila mtu ambaye ni mfuasi ana uongozi uliojificha ndani yake.

2. Sifa ya kila kiongozi ni kuwa na imani ya uongozi.

3. Viongozi bora wanatofautishwa na mtazamo wao chanya, kujijua wao wenyewe na kujiamini.

4. Kila mtu ana mbegu ya uongozi ndani yake, lakini wengi hawana ujasiri wa kuikuza mbegu hiyo.

5. Uongozi wa kweli ni zao la hamasa na siyo kulaghai na kudanganya.

6. Viongozi wa kweli hawatafuti kutawala bali wanasukumwa na mapenzi ya kufanya kile wanachofanya.

7. Jukumu ulilonalo ndiyo linaloamua eneo lako la uongozi.

8. Ujinga mkuu wa mtu ni juu yake binafsi. Kile unachoamini kuhusu wewe, ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako. Hakuna mtu anayeweza kupata makubwa kuliko anachoamini.

9. Mawazo yako yanatengeneza imani yako, imani yako inatengeneza mtazamo wako, mtazamo wako unatawala mapokeo yako ya vitu na mapokeo yako yanatengeneza tabia zako.

10. Uongozi ni upendeleo wa uaminifu unaopewa na wafuasi.

11. Pesa zote duniani zinaweza kukufanya wewe tajiri, mamlaka yote duniani inaweza kukufanya ujione imara, lakini vitu hivi haviwezi kukufanya wewe kuwa kiongozi.

12. Hakuna kitu chenye nguvu kama mtazamo. Mtazamo wako ndiyo unatawala namna unavyochukulia mambo yanayokutokea. Mtazamo wako ndiyo wewe mwenyewe. Kama huwezi kutawala mtazamo wako, utakutawala wewe.

SOMA; Kiongozi Anazaliwa au Anatengenezwa? Jibu Hili Hapa.

13. Kinachowatofautisha wanaoshinda na wanaoshindwa ni mtazamo. Watu wengi wamezipoteza fursa nzuri kutokana na mtazamo waliokuwa nao.

14. Mtazamo ni zao la asili la kujithamini, kujiamini na kujikubali.

15. Hakuna mafunzo yoyote ya uongozi, usimamizi au madaraka yenye nguvu zaidi ya mtazamo.

16. Kila mmoja wetu ameumbwa kusimamia, kuongoza, kudhibiti na kutawala mazingira yanayomzunguka.

17. Wewe tayari ni kiongozi, iwe unatumia uongozi wako au la. Uwe ni masikini au tajiri, mweusi au mweupe, mdogo au mkubwa, mwanamke au mwanaume, una elimu au huna, uongozi upo ndani yako.

18. Kuanza kama mfuasi hakuondoi uwezo wako wa kuwa kiongozi.

19. Uongozi siyo kikundi cha watu wachache, ni kitu ambacho kipo kwa kila binadamu.

20. Ufunguo mkuu wa uongozi ni mtazamo, mtazamo unaanzia ndani ya mtu mwenyewe.

21. Watu wengi siyo viongozi leo kwa sababu walishajishawishi ua kwamba wao siyo viongozi.

22. Kwa sababu viongozi bora wanajijua wao wenyewe kwanza na kusudi la maisha yao, wanayatawala mazingira yao badala ya mazingira kuwatawala wao.

23. Viongozi wa kweli wanapambana kuvuka changamoto wanazokutana nazo na wanakuwa wabunifu kupitia magumu yao.

24. Uwezo mkubwa wa uongozo upo ndani yako unakusubiria wewe uutumie. Ulizaliwa kuongoza, lakini lazima kwanza uwe kiongozi.

25. Uongozi wa kweli unakupa jukumu la kuwapeleka wafuasi kule kusikojulikana na kuweza kuwatengenezea uhalisia mpya.

26. Uongozi ni uwezo wa kushawishi wengine kupitia hamasa inayochochewa na mapenzi na kutengenezwa na maono yanayoongozwa na kusudi.

27. Watu unaowahamasisha wanakuita wewe kiongozi pale wanaposukumwa kushiriki kwenye maono chanya unayowashirikisha, iwe ni maoni ya nchi, kampuni au chochote.

28. Kama hamasa ndiyo ufunguo sahihi wa ushawishi kwenye uongozi, basi kila kiongozi anapaswa kuwa mtu wa hamasa.

29. Uongozi wa kweli ni kupata imani, sababu, wazo au kusudi siyo tu la kuishi nalo, bali la kuwa tayari kufa nalo, lakini liwe la kuwanufaisha wengine.

30. Uongozi mkuu huwa unapatikana wakati wa migogoro binafsi, migogoro ya kiuchumi, migogoro ya kijamii, ya kiimani na hata ya kisiasa.

31. Japokuwa viongozi wana wafuasi, kuwa na wafuasi siyo hitaji kuu la wewe kuwa kiongozi. Mahitaji ya uongozi yanaweza kukutaka uwe tayari kusimama mwenyewe wakati wa mgogoro, kupingwa na hata kukataliwa.

32. Pale unapokuwa na kusudi na maono, yafanyie kazi hata kama ni wewe pekee unayeamini hivyo kwa wakati huo.

33. Viongozi bora wanaifunza uongozi kulitia viongozi wengine, lakini hawajaribu kuiga viongozi hao. Wanathamini kile kitu cha kipekee ambacho kipo ndani yao.

34. Uongozi wa kweli unaanza na wewe ni nani badala ya wewe unafanya nini. Ukishajua wewe ni nani na una nini, chochote utakachofanya, utakuwa kiongozi mzuri.

35. Huhitaji kitu cha ziada ili kuwa kiongozi, hivyo ulivyo, tayari uongozi upo ndani yako. Unachohitaji ni kuanza kutumia uongozi huo.

36. Usitafute ukuu, bali tafuta kuwahudumia wengine na kile kilichopo ndani yako, kwa uwezo wako na watu watakutafuta. Uongozi siyo kutafuta umaarufu, bali kutoa thamani kwa wengine.

SOMA; Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Kiongozi.

37. Njia ya mkato ya kufikia uongozi ni kuwahudumia wengine. Uongozi wa kweli siyo watu wangapi wanakuhudumia wewe, bali wewe unawahudumia watu wangapi. Kadiri unavyowahudumia wengi, ndivyo unavyotengeneza thamani kubwa na kuwa kiongozi mkubwa pia.

38. Kupenda fedha kiasi cha kutojali utu, thamani na ustawi wa wengine ni matumizi mabaya ya nguvu ya kupata utajiri.

39. Viongozi wa kweli ni waaminifu, hawadanganyi wala kulaghai ili kupata kile wanachotaka. Viongozi wa kweli ni wa kweli kwao wenyewe kwanza, halafu ni wa kweli kwa wengine.

40. Kitu muhimu sana kutafuta kwenye maisha ni ukweli.

41. Kutokujiamini na kutokujithamini hupelekea watu kuwadharau wengine na kuwa chanzo cha rushwa, ukandamizaji na hitaji la kuwatawala wengine.

42. Hakuna kitu hatari kama madaraka kuangukia kwenye mikono ya mtu anayejiona wa chini, atawakandamiza sana wengine.

43. Kama unajipenda wewe kweli, utatumia madaraka yako kuwasaidia wengine badala ya kuwaumiza. Vile unavyojiona wewe mwenyewe, ndivyo unavyomwona kila anayekuzunguka. Kama unajiona hufai, unaona kila mtu hafai.

44. Kiini cha uongozi ni kuwapa wengine thamani. Kwa maneno mengine unawapa kitu ambacho kinawafanya kuwa bora na kinawafanya wahusike nacho. Viongozi wa kweli wanawapa watu kitu cha kuamini, wanawapa sababu ya kuishi na kuyafanya maisha yao kuwa na thamani kwa wengine pia.

45. Huwezi kuwaongoza watu kwenda mahali ambapo wewe mwenyewe hujawahi kwenda.

46. Thamani unayoweka kwa wengine ni taswira ya thamani unayoweka kwako wewe mwenyewe.

47. Katika uongozi wako, unahitaji kufikia hatua ambayo unajua kwamba wewe ni wa muhimu. Viongozi wa kweli wanaamini wao ni wa muhimu na wanahitajika na kizazi chao na dunia kwa ujumla.

48. Kile anachoamini kiongozi, ndicho kinachotengeneza asili ya uongozi wake.

49. Uongozi wa kweli unatokea pale mtu anapotumia moto unaowaka ndani yake kuwasha moto ndani ya wengine pia.

50. Kile ambacho hatujui kuhusu sisi wenyewe, ndiyo kikwazo kwetu. Viongozi wanazuiwa na kiasi cha ujuzi wao kuhusu wao wenyewe na dunia kwa ujumla.

51. Unaweza kuigiza kama kiongozi, lakini huwezi kufikiri kama kiongozi kama kweli hujajikubali kuwa kiongozi.

52. Kuchochea imani ya uongozi ndani yako ni maamuzi na wewe pekee ndiye unayeweza kufanya maamuzi hayo.

53. Uongozi wa kweli hauwezi kuwepo kama hakuna kusudi. Kusudi ndiyo linatengeneza jukumu la maisha.

54. Ili uweze kuwa kiongozi ambaye ulizaliwa kuwa, unahitaji kujua kusudi la maisha yako na kuzalisha kile ambacho unapenda kufanya.

55. Viongozi hawafanyi tu kwa sababu wanafanya, bali wanafanya kwa sababu wanajua kwa nini wanafanya. Mapenzi yao yanawasukuma na kuwahamasisha.

56. Viongozi wa kweli hawana kazi/majukumu, bali wana zoezi la maisha yao yote.

57. Viongozi wapo tayari kuweka maisha hao yote kwenye kufikia kusudi la maisha yao.

58. Viongozi wa kweli hawahitaji hamasa kutoka nje ili kuchukua hatua, wana hamasa kutoka ndani yao wenyewe.

59. Uongozi ni sanaa na sayansi kwa wakati mmoja. Ni kitu ambacho tayari kipo ndani yako, lakini bado unahitaji kukiendeleza.

60. Uongozi wa kweli ni matumaini ya kesho na ndiyo unaotengeneza kufanikiwa au kushindwa kwa watu, jamii, taifa na hata dunia kwa ujumla.

61. Kazi kubwa ya kiongozi ni kujiendeleza yeye binafsi kila siku.

62. Viongozi wote wakubwa ni wanafunzi wa maisha, kwa maisha yao yote. Hawafiki mahali na kujiona tayari wanajua kila kitu.

63. Maono ndiyo chanzo cha nidhamu ya viongozi.

64. Viongozi wanajua, kitu cha kwanza kudhibiti ni wao wenyewe.

65. Viongozi wa kweli siyo wafungwa wa tamaduni zao.

66. Viongozi hawafuati njia, bali wanatengeneza njia. Viongozi wanakwenda kule ambapo wengine wanahofia kwenda.

67. Viongozi wa kweli wanajua kila mtu amezaliwa kujaza pengo fulani hapa duniani, wanathamini mchango wa kila mtu.

Je ungependa kuwa kiongozi bora kwenye maisha yako? Anza kwa kuendeleza uongozi ambao tayari upo ndani yako. Uongozi ni kujiamini na kuchukua hatua, anza sasa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita