Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora kabisa.

Chochote tunachotaka, kipo kwenye juhudi zetu. Tuweke juhudi ili kupata kile tunachotaka.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kanuni za mafanikio kubadilika kila siku.
Miaka 100 iliyopita, ili kufanikiwa kifedha ilikuwa ni lazima uwe na kiwanda kikubwa, uzalishe bidhaa ambazo zinahitajika na wengi na uweze kuzitangaza vizuri. Nafasi ya kufanikiwa kifedha ilikuwa ndogo na wachache pekee ndiyo walioweza kuipata.
Lakini leo hii kila mtu anaweza kupata mafanikio makubwa kifedha hata kama hana kiwanda.
Yaani unaweza kupata mafanikio makubwa hata kama huna pa kuanzia. Mazingira yamekuwa rahisi sana kwa kila mtu kuweza kujihusisha na biashara.
Miaka 50 iliyopita kuwa na ajira ilikuwa kipimo kikubwa cha mafanikio. Ilikuwa ni nafasi ya kipekee ya kupata uhakika wa maisha. Kuwa na uhakika wa kulipwa mpaka unapokufa, maana hata ukistaafu ungeendelea kupata mafao.
Lakini leo hii ajira zimekuwa mzigo, ajira zimekuwa changamoto kwa wengi na siyo tena kitu cha kukimbilia na kufurahia.
Miaka 100 iliyopita huduma za afya zilikuwa duni mno, watu walikufa kwa magonjwa ambayo sasa hivi yanayibika vizuri tu.
Miaka 50 iliyopita, kuwasiliana na mtu ilikuwa changamoto kubwa. Ilikuwa ni lazima uandike barua ambayo ingechukua siyo chini ya wiki mpaka imfikie. Lakini leo unaweza kuwasiliana na mtu popote duniani ndani ya sekunde chache na kwa gharama nafuu.
Ninachotaka tutafakari hapa ni kwamba kanuni za mafanikio zinabadilika kila siku. Kilichokuwa vizuri jana kinaweza kisiwe vizuri leo.
Hivyo tusikariri, tuwe tayari kwa ajili ya mabadiliko kila wakati.
Na muhimu zaidi tujifunze kila siku, tuangalie njia mpya za kufanya mambo na tuongeze ubunifu na juhudi zaidi.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki yako,
#KochaMakirita