Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo mazuri. Tumia muda wa leo vizuri rafiki yangu, ukishapita hutaupata tena.

IMG_20170102_073855

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUZAMA NDANI…
Madini yenye thamani kubwa huwa hayapatikani kwa urahisi juu ya ardhi, badala yake yapo chini ya ardhi. Hivyo iki kuyapata lazima mtu uchimbe na kuzama ndani ndipo uweze kukutana na madini hayo.
Siyo juu juu kwa urahisi rahisi tu unaweza kuchota madini kama unavyochota mchanga. Unahitaji kuchimba, unahitaji kuzama ndani zaidi ili kupata thamani hiyo kubwa.

Sasa hilo haliishii kwenye uchimbaji wa madini pekee, bali linakwenda kwenye kila eneo la maisha yetu.
Thamani inapatikana ndani zaidi, baada ya kuzama zaidi, na siyo juu juu kwa kugusa gusa vitu.
Kwenye biashara unapata mafanikio pale unapozama ndani zaidi, pale unapoijua biashara unayoifanya nje ndani na kuifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
Hivyo pia kwenye kazi, hakuna anayefanikiwa kwa kufanya mambo juu juu, unahitaji kwenda ndani zaidi, unahiyaji kuzama na kujua zaidi kuhusu kile unachofanya.

Hivyo rafiki yangu, asubuhi ya leo ondoka na azimio hili; kwenye kile ambacho umechagua kufanya, ZAMA NDANI ZAIDI, kijue vizuri kuliko mtu mwingine yeyote, jua wapi thamani ilipo na weka mkazo hapo, zama ndani na utaibuka na madini yenye thamani kubwa sana.

Mafanikio yanakuja pale unapochagua kitu (chochote) na ukawa tayari kuzama ndani zaidi, kukijua vizuri na kukifanyia kazi.
Chagua kitu, jitoe, zama ndani na jifunze kila siku.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki yako,
#KochaMakirita