Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera sana kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Tutumie nafasi hii ya leo vizuri rafiki yangu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kuongezeka busara na siyo kuongezeka uzito.
Watu wengi, wanapokuwa watu wazima, kitu pekee wanachoongezeka ni uzito.
Wanaongezeka uzito haraka kwa sababu ni rahisi kufanya hivyo.
Kwa kuwa tu mzembe unaweza kuongeza uzito mkubwa iwezekanavyo.
Kwa kukosa nidhamu kwenye ulaji na ufanyaji wa mazoezi, uzito unaongezeka mara dufu.
Lakini kipo kitu muhimu sana ambacho mtu angepaswa kuongeza kadiri anavyokuwa mtu mzima. Kitu hicho ni busara. Lakini wengi hawawezi kuongeza busara kadiri wanavyokuwa watu wazima kwa sababu kuongeza busara ni kazi. Na kazi ambayo mtu anahitaji kuifanya, hakutokei tu kizembe, mtu anahitaji kuweka juhudi za kujifunza na kufanya mambo mapya.
Hivyo rafiki yangu na mwanamafanikio, azimio lako iwe kuongezeka busara na siyo kuongezeka uzito.
Kuongezeka uzito ni hatari kwako, unakaribisha magonjwa hatari na sugu.
Kuongezeka busara kuna manufaa makubwa kwako, unaongeza nafasi yako ya kuwa na maisha bora zaidi na mafanikio pia.
Ongezeka busara kila siku, kwa kujifunza mambo mapya, kujaribu mambo mapya na makubwa, kukabiliana na changamoto unazokutana nazo kila siku na kuchagua kutumia kila kilichopo mbele yako kama fursa ya kukua zaidi.
Usikimbilie mambo rahisi ambayo hayana manufaa kwako, kama kuongezeka uzito. Badala yake weka juhudi zako kwenye mambo magumu ambayo yatakuwa na manufaa kwako, kama busara.
Nikutakie siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki yako,
#KochaMakirita