Homgera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana na ya kipekee kwetu.
Ni nafasi nyingine bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi.

img-20161217-wa0002
Rafiki iendee siku ya leo kwa KUTHUBUTU, USHINDI NA SHUKRANI.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu HAKUNA NJIA NYINGINE.
Iko hivi rafiki, mara nyingi watu huwa wanazoea kufanya kitu kimoja kwa muda mrefu kiasi cha kufikia hatua ya kuamini kwamba hakuna njia nyingine ya kufanya hivyo isipokuwa ile waliyozoea.
Watu wanakuwa wamezoea kitu hiko kimoja na hawajawahi kupata picha kwamba kuna njia nyingine inawezekana kufanya bora zaidi.
Hii ni hali ambayo imewazuia wengi kuchukua hatua za kuboresha maisha yao. Inawafanya watu kuendelea kufanya kile walichozoea kufanya hata kama hakina manufaa kwao.

Asubuhi ya leo hebu tafakari kwa makini ni vitu gani umezoea kufanya kwenye maisha yako kiasi kwamba umejiaminisha hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo unayotumia?
Je ni kwenye kuingiza kipato? Kwamba umezoea njia moja tu, labda mshahara au biashara fulani, kiasi cha kuamini hakuna njia nyingine?
Je ni mbinu zako za kufanya kazi au biashara ambazo zimeshapitwa na wakati lakini unazing’ang’ania kwa sababu ndiyo umezizoea?
Au ni aina ya maisha unayoishi sasa, ambayo umesharidhika nayo na kuona huwezi kupiga hatua zaidi ya hapo?
Yatafakari maisha yako na uone wapi panakurudisha nyuma kutokana na imani ja mazoea kwamba hakuna njia nyingine.

Anza kufikiri tofauti,
Anza kuona wingi wa njia za kukufikisha kule unakotaka kufika.
Na anza kujaribu njia za tofauti za kufika unakotaka kufika.
Anza leo hii, kwa kujaribu vitu vidogo, anza kwa KUTHUBUTU kuchukua hatua ambayo hukuwahi kuchukua. Anza kwa kutengeneza USHINDI mdogo mdogo leo. Na utaona njia nyingi za kutoka hapo ulipo.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
#KochaMakirita