Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

IMG_20170102_073855
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA. Tunaweza kufanya makubwa kwa msingi huu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu JANA NA KESHO.
Hizi ni siku mbili ambazo zimekuwa zinapoteza maisha yetu kila siku.
Siku hizi mbili zimekuwa zinaiba muda wetu muhimu tulionao kwa matumaini ambayo hayawezekani au hatutayafanya.

Kwanza huwa tunaanza na jana,
Kwa kuangalia mambo tuliyofanya au kutokufanya,
Na kuanza kujiambia NINGE….
Tunaona namna ambavyo hatukuzitumia fursa tulizopata vizuri.
Tunaona namna ambavyo tungeweza kufanya kwa ubora zaidi.

Kibaya zaidi, tunaenda kesho,
Hapa ndipo tunajiambia NITA….
Tunaangalia yale ambayo ni muhimu kwetu kufanya na kujiambia kesho nitafanya hivi.
Tunaangalia kule tunakokwenda na kujiahidi kesho tutafanya.

Cha kushangaza zaidi, huu muda tulionao sasa, hatuutumii, tunasubiri kesho ifike tuseme JANA NINGE…. na kesho hiyo tena tupange kesho yake.
Unaona namna ambavyo tunachagua kupoteza muda tulionao?

Sasa dawa ni hii; chochote unachopanga kufanya, anza kukifanya mara moja na chagua kukifanya kila siku, KILA SIKU, na itakuwa vizuri zaidi ukakifanya kwenye muda ule ule.
Achana na hadithi za JANA NA KESHO,
Mpango mzima ni LEO, fanya leo, tumia muda huu ulionao sasa.

Hata wahenga walisema, LEO NDIYO LEO, ASEMAYE KESHO NI MWONGO. Usiwe mwongo, fanya mambo leo.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.