Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kweru kwenda kuweka juhudi kubwa na kutegemea kupata matokeo bora kabisa.

Ni siku nzuri kwetu kwenda kujifunza mambo mapya na kujaribu mambo ambayo hatujawahi kufanya.
Tunakwenda kuweka NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA siku hii ya leo kwa sababu huu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kuanza wewe,
Chochote unachotaka watu wakufanyie kwenye maisha yako, inabidi uanze kukifanya wewe.
Kwa sababu wanachokufanyia watu, ni kile ambacho unafanya wewe mwenyewe.
Yaani watu wanakupa kile ambacho unatoa, hivyo ukitaka wakupe kitu cha tofauti, anza kutoa kitu cha tofauti.
Kama unataka watu wawe waaminifu kwako, anza kuwa mwaminifu wewe mwenyewe. Kama umezungukwa na watu ambao siyo waaminifu basi jua umewakaribisha wewe mwenyewe, kwa kutokuwa na uaminifu.
Kama unataka watu wanaokuzunguka wawe wachapakazi, hasa wale ambao ni wasaidizi wako, anza kuwa mchapakazi wewe. Wanachofanya wao ni kile unachofanya wewe.
Kama unataka watu wawe makini, anza kuwa makini wewe.
Chochote watu wanakupa sasa, ni sawa na wanakurudishia kile unachotoa. Hivyo kama unataka bora zaidi, anza kutoa kilicho bora zaidi.
Kuwa vile unavyotaka watu wakufanyie, na utawakaribisha wale wanaoweza kufanya kile unachofanya wewe.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.